ADVERT

27 August, 2008

Taarifa kwa Umma juu ya Sera Mpya ya Vijana na Msimamo wa TYVA katika Sakata la Usafiri kwa Wanafunzi!

27TH Agosti, 2008
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
MJADALA KUHUSU SERA MPYA YA VIJANA TANZANIA
“JE SERA MPYA IMEAKISI MAHITAJI NA CHANGAMOTO ZA VIJANA WA SASA?”

Ndugu zangu waandishi wa habari,
Awali ya yote napenda kuwashukuru kwa kuitikia mwito wangu wa kuja kuzungumza nanyi. Nasema hivi kwa sababu kwa nguvu zenu hususan katika taaluma yenu hii ya habari na umuhimu wake mkubwa katika kuelekea jamii huru, ahaki, yenye uwakilishi bora mathalani wa vijana kazi ambayo mnajitahidi kila kukicha.
Asasi ya Dira ya Vijana Tanzania [Tanzania Youth Vision Association] kwa kushirikiana na shirika la kimataifa la toka Ujerumani Friedrich Naumann Foundation [FNF] inakusudia kuitisha mkutano wa vijana kujadili suala la sera mpya ya vijana ya mwaka 2007 iliyozinduliwa mwaka 2008.
Mjadala huu ni mfululizo wa mijadala tuliyoipa jina la DIRA ambayo tumekuwa tukiifanya kwa takribani miaka sita [6] sasa ikitendeka karibu kila mwezi chini ya udhamini wa mshirika wetu “Partner” FNF kama uwanja mpana wa kukuza demokrasia, kushawishi, na kutetea kupitia uhuru wa kujadili, kupata taarifa sahihi, na hatimaye kutoa fikra pevu katika masuala nyeti ya nchi ambayo kwa namna moja pia huwaathiri na kuwagusa vijana kusaidia utungwaji, mrekebisho na utekelezaji wa sera kadha wa kadha na maamuzi.
Mjadala wa DIRA utafanyika kesho kutwa, siku ya Ijumaa ya tarehe 29 Agosti, 2008 kuanzia saa mbili asubuhi mpaka saa saba mchana katika Hoteli ya Rombo Green View, Sinza. Mada ya mjadala huu itajikita kujibu swali la, “Je Sera mpya imeakisi mahitaji na changamoto za vijana wa sasa?” Kutakuwa na mada itakayochambua sera ya vijana ikiakisi changamoto kadha wa kadha za vijana wa Tanzania itakayotolewa na Ndugu Chambi Chachage mtafiti na mchambuzi wa sera wa kujitegemea, ikifanya rejea katika mikataba na makubaliano kadha wa kadha ya kitaifa na kimataifa ambayo nchi yetu imeridhia. Nakutoa uwanda mpana wa mjadala kwa washiriki kuweza kutoa uchambuzi mpevu na fikra mbadala kujibu swali hili yote yakilenga katika kuelekea ustawi bora wa nchi yetu.
Mjadala wa DIRA unakusudiwa kuwaleta pamoja vijana takribani hamsini kutoka kwenye asasi za vijana, vyuo vya elimu ya juu, shule za sekondari, vyama vya siasa, vijana walioko makazini na mitaani. Vilevile umealika wadau wa masuala ya vijana mathalani serikali kwa kupitia Wizara ya Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana, Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia watoto[pamoja na vijana] UNICEF.Vyombo vya habari vinaalikwa kuja kushiriki na kutoa taarifa kwa vijana wengi zaidi nchini ambao nao wanahitaji kupata taarifa hii sahihi.
Shabaha yetu ya kufanya mijadala ya DIRA ni kuwajengea uwezo vijana waweze kushiriki ili washirikishwe kikamilifu katika kutoa fikra, maoni, mitazamo katika masuala nyeti ya nchi ambayo yanasaidia sana kujenga na kuboresha sera, programu na mipango katika nchi yetu.
Sisi Tanzania Youth Vision Association [TYVA] ama Asasi ya Dira ya Vijana Tanzania inajukumu kubwa kama asasi ya kiraia ya vijana, isiyo ya kiserikali na isiyofungamana na itikadi, kikundi wala chama chochote cha kisiasa kujenga mazingira ya jukwaa la mijadala kwa vijana na kuchambua kimakini sera, programu na utekelezwaji wake ikiwa mwanya wa kusambaza taarifa hizi adhimu.
Ifahamike asasi ya TYVA toka kusajiliwa kwake mwaka 2002 imekuwa ikitetea na kushawishi mapitio na marekebisho ya iliyokuwa sera ya vijana mwaka 1996 huku tukitoa maoni na mitazamo yetu hususan changamoto na mahitaji halisi ya vijana. Hivyo hatuna budi kuichambua sera hii mpya ya mwaka 2007 na kutanabaisha kwa kina uwezo, fursa, changamoto na udhaifu ama mapungufu yake mapema ili vyombo mbalimbali vya utekelezaji viweze kujenga mipango na programu bora za utekelezaji wake zikishirikisha mahitaji yote halisia ya vijana.
Utekelezaji bora wa sera hii unaweza fikiwa vyema ikiwa mambo kadhaa kujadiliwa kwa kina kuelekea kufanikiwa huko. Kwa kuwa mjadala wa DIRA utayachambua baadhi ya mambo haya na kuja na mtizamo wa vijana nakusudia kusema mambo machache tu katika hili ili isaidie kuibua mijadala kama hii mahala pengine.
Mjadala huu utakuwa uwanda mpana sana wa kujadili mikataba ambayo nchi yetu imeridhia katika kuelekea ustawi wa vijana nchini na duniani kwa ujumla mathalani Mkataba wa Vijana Afrika “African Youth Charter” kama ulivyoridhiwa na Tanzania Juni 2006. Mpango wa Dunia wa Umoja wa Mataifa kwa Vijana wa mwaka 2000 na kuendelea “United Nations World Programme of Action for Youth to the year 2000”.
Bila shaka mjadala utaweza kugusia changamoto ambazo hata katika sera baadhi zinaainishwa mathalani kutokuwepo fursa sawa katika kujitengenezea kipato, mali, na madaraka, umaskini na njaa, kutoshiriki na kushirikishwa kikamilifu katika vyombo vya kutengeneza sera na kupitisha maamuzi, ujinga na mfumo mbaya wa elimu, ukosefu wa ajira, kuathirika na kuathiriwa na VVU/UKIMWI, unyanyasaji wa kijinsia na ubaguzi, ugumu katika kupata huduma za afya na taarifa, uhitaji wa uwepo wa baraza la vijana. Haya ni baadhi tu, mjadala utakuwa kioo cha demokrasia kwa kuruhusu utoaji wa maoni na mitazamo kufuatana na uwakilishi.
Ndugu waandishi wa Habari,
Naomba sasa nizungumzie na kutoa msimamo wetu kuhusu sakata la wanafunzi hususan baada ya ongezeko la nauli.
Tumeweza kushuhudia Taifa letu likipitia hali ngumu sana ya mabadiliko hasa yakiakisi mfumuko na ongezeko la bei ya mafuta na kupelekea kutokana na sera za nchi kupanda kwa nauli katika usafiri.
Hali ambayo imeongeza mzigo katika matatizo ya hali ngumu ya upatikanaji wa usafiri kwa wanafunzi hususan waishio mijini ambao wamekuwa wakitegemea huduma hii kuwafikisha mashuleni na kuwarudisha majumbani.
TYVA inatoa rai kwa serikali kupitia Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kuandaa mkakati madhubuti wa kutatua kero hii kwa wanafunzi mathalani kutengwa kwa mabasi ya wanafunzi jambo ambalo litasaidia hata ubora wa juhudi za serikali katika kukuza na kuboresha elimu nchini kupitia mikakati kama MMEM na MMES.
Tunahitaji kufungua uwanja mpana kwa uwepo wa mjadala juu ya uboreshwaji wa miundo mbinu na huduma ya usafiri kwa wanafunzi nchini ambapo unaweza ibua maoni, hoja na fikra mbadala zitakazoweza boresha hali ya usafiri kwa wanafunzi ambayo sasa ipo katika hali mbaya sana.
Tunashawishi wamiliki na watendaji wa vyombo vya usafiri nchini vitenge nafasi maalumu kwa wanafunzi ambazo zitafahamika kabisa japo viti viwili kwa mabasi madogo almaarufu kama “vipanya” na viti vinne kwa mabasi makubwa. Hii iende sambamba na upakiwaji wa wanafunzi wa kutosha kwenye mabasi hususan muda wa asubuhi na alasiri au jioni.
Tunashauri uwepo wa uhudumiaji wa ukarimu, upendo na kujali kati ya wanafunzi na watendaji katika vyombo vya usafiri. Kwani TYVA ina amini kwa uwepo wa hali ya upendo, ukarimu na kujali kwa wanafunzi toka kwa watendaji wa vyombo vya usafiri utatatua kwa kiasi kikubwa migogoro na unyanyasaji ambayo hujitokeza mara kwa mara kwa wanafunzi ambayo wakati mwingine mwisho wake umekuwa wa madhara makubwa si tu kwa wanafunzi hata watendaji hawa wa vyombo vya usafiri.
TYVA inaitaka wizara husika ifanye juhudi za dhati na za haraka kusimamia uboreshwaji wa huduma ya usafiri kwa wanafunzi kwani tatizo hili limemea na kuoata mizizi jambo ambalo linaathiri sana mwenendo mzima wa jamii yetu hususan uibukaji wa kizazi chenye matabaka, chuki, visasi, uhasama toka kwa wanafunzi wanaonyanyasika na kutaabika kwa upatikanaji wa usafiri.
Tanzania Youth Vision Association [TYVA] ama Asasi ya Dira ya Vijana Tanzania ni asasi ya vijana, isiyo ya kiserikali na isiyofungamana na itikadi, kikundi wala chama chochote cha kisiasa. TYVA ilianzishwa mnamo mwaka 2000 na kupata usajili wakitaifa mwaka 2002 kwa hati ya usajili nambari SO.NO. 11454.
Dira yetu: Kuwa na jamii huru, ya haki, ya kidemokrasia na yenye amani ambayo ina ushiriki hai wenye manufaa kwa vijana.
TYVA imejitolea kwa dhati kukuza uwezeshaji na kujing’amua kwa vijana kwa kuw na programu fahamu, zenye kujenga uwezo na mitanao yenye kulenga vijana, yenye kuzingatia jinsia, rafiki kwa mazingira na zipatikanazo kwa ufanisi na kwa vijana walio katika mazingira magumu.
Asanteni Sana Kwa kunisikiliza!
Mungu ibariki Tanzania
Imetayarishwa na;

……………………
Michael Dalali
Katibu Mkuu Taifa-TYVA
0755-45 97 83.

No comments: