ADVERT

24 February, 2008

TAMKO LA KUPINGA MUSWADA WA ONGEZEKO LA GHARAMA ZA ELIMU

TANZANIA YOUTH VISION ASSOCIATION

TAMKO LA KUPINGA MUSWADA WA ONGEZEKO LA GHARAMA ZA ELIMU YA JUU

Tanzania Youth Vision Association [TYVA] ni Asasi ya Kiraia ya vijana iliyosajiliwa mwaka 2002 [S.O.NO.11454] inayotetea uwepo wa ustawi wa haki, demokrasia na jamii huru yenye ushiriki imara wa vijana.

TYVA imeshtushwa na kusikitishwa kwa mapendekezo ya Tume ya Uchunguzi juu ya Uendeshwaji wa Vyuo Vikuu na Baraza la Chuo Kikuu cha Dar-Es-Salaam kwa serikali, kinatarajia kupandisha ada kwa kozi zote zinazotolewa chuoni hapo kuanzia muhula wa masomo wa Septemba mwaka huu kwa wanafunzi wapya na wanaoendelea na masomo.

Mchanganuo huo uliowasilishwa unaonyesha wanafunzi wanaoendelea na masomo watatakiwa kulipa kati ya Tsh 1.3 hadi 2.5 milioni kwa mwaka kutegemeana na kozi wanazosoma kwa ajili ya ada ya masomo [tuition fee].Mfano: Kozi za Kitivo cha Sayansi ya Jamii [isipokuwa Uchumi na Ualimu] itapanda toka Sh 722,000 hadi Sh 1 milioni wakati Kitivo cha sheria watatakiwa kulipa Sh 2.5 milioni.

Ikimbukwe licha ya kuwepo kwa Bodi ya Mkopo bado kuna makundi ya wanafunzi wanaotakiwa kulipa asilimia ya ada kutokana na kundi la tathimini walilopo, Mfano: asilimia 40.Lakini pia wapo wanaojilipia wenyewe kutokana na kushindwa kwa Bodi ya Mikopo kuwalipia.

Gharama zote hizi za kupanda kwa elimu wanaendelea kubebeshwa wananchi ambao tayari wanaathirika vibaya sana na kupanda kwa gharama za huduma za kijamii mathalani umeme na kiujumla hali ya maisha kuwa juu.

Ikumbukwe kuibuka kwa migomo mnamo mwaka jana kupinga ulipwaji wa asilimia 40 za ada kwa wanafunzi hali ambayo iliathiri sana kiwango cha elimu ya juu. Hali ambayo serikali inaweza kuiepuka kwa kutoridhia mapendekezo ya kikandamizaji kwa wananchi kama haya.

Ongezeko hilo likiridhiwa litaathiri sana upatikanaji wa elimu nchini na kupelekea wananchi wa kawaida kutoweza kumudu gharama za hali ya juu za masomo katika ngazi mbalimbali kama shahada ya kwanza, shahada ya pili "uzamili" na kuendelea.Kitu kitakachozalisha taifa lenye wasomi wachache na wanaotoka tabaka la juu.


TYVA inashawishi Chuo Kikuu kifikirie tena juu ya pendekezo hilo la ongezeko la gharama za ada na kutafuta namna ya upatikanaji wa ruzuku wa kukiendesha bila kuathiri upatikanaji wa elimu.

TYVA inashauri serikali kutoridhia mapendekezo toka Tume ya Uchunguzi juu ya Uendeshwaji wa Vyuo Vikuu na Baraza la Chuo Kikuu cha Dar-Es-Salaam juu ya ongezeko la viwango vya ada kwani litaathiri sana sekta ya elimu nchini na kwa wananchi kwa ujumla.

Bado kuna mianya na fursa nyingi za rasilimali ndani ya nchi ambazo endapo zikitumiwa vyema huduma nyeti kama ya elimu na nyingine nyingi zinaweza kutolewa kwa Taifa bila kuwepo kwa vizingiti, urasimu na matabaka kwenye upatikanaji.

TYVA inasisitiza hitaji la serikali kuongeza juhudi katika kuwekeza katika elimu kwa vijana ili kuweza kuwajengea uwezo tayari kukabili mazingira magumu yaliyopo ya ufinyu wa upatikanaji wa ajira rasmi na kujenga Taifa lenye wataalamu wa kutosha.

Michael J. Dalali
Katibu Mkuu Taifa
Tanzania Youth Vision Association
Cell: 0755- 45 97 83
0732- 09 09 09
Email: tyvavijana@yahoo.com

Cc: Vyombo vya Habari
Asasi za Kiraia

No comments: