ADVERT

27 July, 2011

Yuda kipenzi changu, waniangusha

Na. Churchill Shakim


Alikuja kwangu mchana kweupe.

Mikono kaifumbata nyuma, kwa unyenyekevu mwingi. Mwendo wake taratibu.
Kanikuta nimechakaa, nimechakazwa na kazi za shamba. Jasho lanivuja na uchovu wenye kuudhi.

Nakumbuka, tena ni mchana wa jua kali siku ya alhamisi. Jua lingali uchi muda huo. Nani mwenye kuthubutu kutazama uchi wa jua! Hakuna, ndio maana hatulitazami tusijepata laana na upofu.

Mtu huyu mwerevu nikamkaribisha aketi kwenye kigoda changu. Nyumba yangu haina viti. Hakutamani kuketi kitini bali vumbini. Eti hapa chini patamtosha. Hajali vumbi. Haoni shida mavazi yake kuchafuka. Mbona nasi twakaa chini hata jamvini hatumudu!

Nikampa maji ya kata apoze koo, naye akapiga funda mbili za maji ya kisima. Maji adimu nyakati za kiangazi. Mtu huyu mtanashati, Mgeni wangu msaliti nikampenda. Nikapenda haiba yake. Hapo akanivuta kama sumaku.

Nikampisha aseme kilichomleta. Shauku imenikaa moyoni kama kijana anayejiandaa kwenda jandoni. Nikavuta usikivu. Jadi yangu uvumilivu. Si vema kumkatiza. Akasema zaidi, nami nikasikiliza. Sikio haliozi kwa kusikia wala halichakazwi kwa maneno. Kasema mengi na mengine nimesahau maana bashasha iliyonijaa kila baada ya kauli zake, sikutaka hata aendelee zaidi. Jakamoyo humaliza hadithi kabla mtambaji hajafika tamati.

Nikapiga mbinja majirani wafike, nao wasikie habari ya mtu mwema. Analeta tumaini katika mioyo iliyopondeka. Wanaume wakaimba kumsifu, vijana wakamwita rafiki, wakina mama wakasema ni mtanashati. Akapendwa na wote isipokuwa Chakubimbi. Watu wakamkebehi Chakubimbi, ‘ahh, tushamzowea huyu. Kila jambo kwake baya.’ Mwenye kuzomea kazomea, Chakubimbi hakujali, akasonya akaondoka. Nakumbuka moja alilosema pembeni ili mgeni wangu asisikie. ‘Wajinga ndio waliao’. Nikatahayari, ‘eti ngoma muichezayo mtakujalia kwa mdundo huohuo.’

Nikampa mgeni wangu alichotaka, naye kanipa ahadi. Ahadi ya mambo mema siku si nyingi. Tena kasema itakuwa punde kabla ya juma kupita. Atarejesha mara thenashara, anipe zaidi ya ujira. Wengine wakatamani ujira bila ajira na wengine ajira bila ujira. Nikawaza ulikuwa wapi siku zetu za masumbuko? Siku za kuhangaika? Nyakati za kufunga mkanda hasa kwa kuwa kiuno chenyewe kilishakongoroka kwa dhiki na kuacha makongoro kama mijengo ya pagale?

Shamrashamra zikapita na mgeni wangu kaondoka. Nami nikampenda. Akaniachia picha yake, kama ishara ya kumkumbuka. Akanipa na kipande cha kaniki chenye sura yake kama agano la ahadi yetu.

Ahadi ni deni ama ahadi ni duni!

Siku za matumaini zilikuwa nyingi. Nikatamani nimwone tena kama ilivyo ahadi yetu. Mara kimya kikatanda ila nikavuta subira zaidi. ‘Essabr’ muftah elfa rah’, mambo mema huwangoja wale wenye kusubiri labda tutafsiri hivyo maneno haya ya kiarabu.

Subira yavuta heri ama subira yavuta shari!

Nikasikia mgeni wangu, yule Yuda anatanga. Nimesema tanga, si matanga. Kutangatanga kwake ndiko kunakoniletea mimi matanga. Wakasema wamemwona pwani, chombo chake kilikuwa kerezani kinatengenezwa akingoja upepo. Keshapandisha tanga. Nikauliza kanunua lini jahazi? He! Sina habari, mambo yako wazi nami napitwa tu na nyakati. Ana kundi la maswahiba, wote wamo chomboni. Pepo zinawabeba kusi na kaskazi, kumwona tena mi siwezi. Siku nyingine kaonekana kasrini, akiwapokea wengi kutoka mbali. Wazito hasa.

Siku zinapita, mbona tena simwoni? Amesahau ahadi yetu? Mkopo niliompatia alisema atanilipa sawia, sasa imekuwaje tena! Tumekuwa mbali mimi na yeye kama Magharibi na Mashariki. Amenifanya iliki, mara kwenye chai mara kwenye wali, mara kwenye maandazi lakini anasifiwa mpishi na utamu wa wali. Kweli iliki haipikwi bila chenginecho kuwepo. Upuuzi mtupu.

Hapa nilipo nina hasira sana.

Namlaani, eti ‘nitamkomesha’. Si atakuja tena. ‘mchama ago hanyeli, huenda akauya papo’. Wazaramo nasi kwa misemo tu! Eti ukihama kambi usiinyee huenda ukarudi tena hapohapo. Mi na yeye tuna nasaba, wote wazaramo. Kwetu pwani.

Chakubimbi kanisikia kanicheka. ‘We bwana utakuwa mwehu bure. Tangu lini ukalificha jua kwa kipande cha kaniki? Dua la kuku hilo halimpati mwewe.’

Kaniudhi, nikamjibu kwa dharau, ‘nitafanya niwezalo. Siwezi kuchelewa safari kwa kukaza gidamu ya kiatu. Nitamshitaki barazani. Wote mnajua agano letu.’

Nilijua siwezi na sina thubutu hiyo achilia mbali kujiamini. Hivi kweli kesi ya mende nimfanye jogoo kuwa hakimu? Hata nikiweka wakili bado atakuwa tetea, naye atammaliza kabla ya kufika barazani. Lazima kuwe na njia nyingine ya kudai deni langu. Nayo ni kusamehe. Na akija tena simpokei wala kumkopesha.

Ghadhabu, ghadhabu zingekuwa zinaua kwa nilivyoghadhibika ningeshapasuka. Ila nikikumbuka siku ile ya kwanza kukutana na mgeni wangu najicheka tena. Eti, si mimi nilipita nyumba kwa nyumba nikatandaza habari zake. Nakumbuka siku nilipomshika mkono, nikashituka kama kulikuwa na nguvu ya umeme. Nikatamani nisioshe kiganja nisijefuta baraka. Sasa iweje leo nimlaumu. Kosa ni langu ama lake? Nani msaliti kati yetu? Nimejisaliti mwenyewe. Hakunishurutisha. Alinitongoza nikakubali, ila niseme kulikuwa na ghiliba ndani yake. Mtongozaji mwenye ahadi zaidi ya urefu wa kanzu yake anafaa kutiliwa shaka. Lakini mi nilikuwa mpofu kwa mapenzi. Nilisukumwa na haiba na wajihi wake na sikuwa na tafakari.

Sasa yanipasa kukata mkono ili kuunga wajihi. Hii ni ngumu sana. Najua siku itafika atakuja na nitamtolea uvivu.

Waswahili husema, ‘mwenda tezi na omo, marejeo ni ngamani’. Mara Jumatano hii hapa. Hebu kumbuka, Alhamisi ya juma lililopita mpaka leo Jumatano ni siku ngapi zimetimia? Nisaidie hesabu hii rahisi kwako, we mwenzangu umesoma shule ya kisasa ya Mtakatifu nani sijui. Mwalimu wangu mie wa hisabati alikuwa na gubu, haishi maudhi mwanamama yule hasa ikifika mwisho wa mwezi. Mshahara hajapata eti karani anasema mishahara ya walimu imeibwa. Iliwekwa kwenye sefu lakini kakuta imevunjwa. Hivi mshahara wa mtu si mpaka autie mkononi ndio uwe wake? Sasa kama umeibwa ukiwa huko maghorofani unakuwaje tena wa mwalimu?

Ujue hapo mwalimu wangu atarudi amenuna na akichanganya na yake atapiga bakora darasa zima bila kosa la maana. Kisha ndio anifundishe hisabati. Nitampenda kweli yeye na somo lake? Ukiachilia mbali zile siku nyingine ambazo hakuwepo alikuwa wilayani na kwenye semina. Ama sikuwa darasani nilikwenda kuteka maji ya mwalimu mkuu.

Basi mgeni akawa Yuda akaja siku hiyo ya Alhamisi, safari hii si kama mwanzo. Kaja na hubiri mpya. Injili yenye majigambo kuwa kafanya mengi hata kama hatuyaoni.

Kanikumbusha kuwa yeye ni mwanadamu, hana uwezo wa kiMungu eti atake jambo litokee ghafla.

Nahisi kama kuna kitu kimenikaba kooni. Sijui ni woga, ama hasira, ama ghadhabu! Natamani nimkumbushe deni langu lakini siwezi hata kumsogelea. Safari hii hanijali sana maana kuna wengine watamsikiliza. Chakubimbi kanicheka lakini sasa namwelewa.

Wengi wametoka vichwa chini. Na wengine wanasema hawaoni mwanga tena hata kama ni mchana wa jua kali. Na wengine wachache sasa wanamwelewa Chakubimbi. Lakini ulimwengu hauishi mastaajabu. Eti tena amepata alichotaka. Waliompa wanasubiri tena juma lijalo arejeshe.

Chakubimbi ananiambia turudi zetu nyumbani giza linaingia. Lakini nataka kupitia dukani ninunue kibiriti kwa shilingi hii ya mwisho iliyobaki mfukoni nikawashe taa. Namaizi kuwa sitaweza kuwasha taa bila mafuta. Hakuna mafuta kila mahali. Kijiji gani hiki jamani? Leo pia nalala gizani.

Wengine wananikebehi eti natarajia kulipwa makubwa, thenashara, kwa kipimo gani hasa?

Ila nawakumbusha kuwa, licha ya kunikebehi kwenu, bado..
 Tutahitaji kupeleka watoto katika shule isiyo na walimu wala vitabu.
 Hospitali isiyo na dawa wala mganga aliyefuzu vyema lakini imejaa maboksi ya kondom kuliko dawa za magonjwa mengine.
 Kulipia haki sababu wapo walioinunua kabla yetu.
 Kuishi gizani mpaka Mungu akipenda kuleta mvua ili tupate mwangaza.

Chanzo: http://www.facebook.com/notes/churchill-shakim/yuda-kipenzi-changu-waniangusha/10150290316899881

1 comment:

Anonymous said...

Hello, I like it, kwanini usiiweke katika magazeti ndugu yangu ili wengi waweze kuiona hii kazi??? Kuna haja ya kutumia njia mbali mbali ili tuweze kufika huko tunakotaka kufika.