ADVERT

12 July, 2011

Wawepo wasiwepo mambo safi!

Kikao cha nne cha bunge la kumi kinachoendelea mjini Dodoma kinaibua maswali mengi hasa katika muenendo wa ushiriki finyu bungeni. Ni miezi takribani tisa toka wabunge hawa watangazwe washindi baada ya mikiki mikiki ya kipindi cha kampeni ambako walijinadi kuhitaji kutumwa kwenda kuwakilisha wananchi wengine katika chombo cha maamuzi.

Hivi karibuni, naamini wengi wa wananchi ambao wamekuwa wakifatilia vikao vya bunge ni mashahidi wa ufinyu wa ushiriki wa wawakilishi wetu katika kikao cha bunge. Hali hii inaibua maswali mengi sana miongoni mwa wananchi wapenda maslahi ya nchi.

“Hivi bunge hili linaendeleza tabia kama ya bunge lililopia (yaani bunge la tisa)?”, mwingine akahoji; “hivi kuna sababu gani hasa zinazowafanya wabunge kutomudu kushiriki kikao cha bunge wakati hiyo ni sehemu yao ya kazi” ni miongoni mwa maswali ambayo huwa nakumbana nayo toka kwa wananchi waangaliapo bunge na kuonyeshwa kupitia televisheni viti vilivyotupu.

Hakika inaibua sintofahamu ambayo nadhani ni wabunge wenyewe wanaweza kuichambua kwa kina.

Lakini haraka haraka mawazo yanayoweza kuja akilini ni pengine; Mosi, kikao cha bunge kimekuwa kirefu sana kuliko vile ambavyo wabunge wanahimili kutulia kukishiriki kikamilifu. Hii inaweza kupimwa na kulinganisha na vikao ambavyo vitatu vya vyanzo ambavyo havikuzidi mwezi kuliko kikao cha nne cha bajeti ambacho ni takribani miezi mitatu.

Kwa upande mwingine inawezekana wabunge wa bunge la kumi tayari wameshazoea muenendo na utendaji kazi wa bunge, ambako imewafanya kujua namna ya kuishi bungeni “kiujanja ujanja”. Hii inakuwa ni miongoni mwa tabia inayotokana na kuanza kuzeoa kitu na hasa mazoea yaliyopitilia yenye kumfanya mtu kujisahau.

Kufahamu huku inaendana na kujua namna gani ya kukwepa rungu la sheria na kanuni kumwangukia baada ya kuivunja mathalani; kanuni zinataka mbunge kuhakikisha hakosi mikutano mitatu mfululizo (siyo vikao). Kanuni zinamwangaza mbunge aliyepo katika kikao hasa katika kipindi cha kupitisha maamuzi ambapo suala la akidi inapaswa itimie.

Hapa ndipo tunaona baadhi ya wabunge tena wakuchaguliwa wanasaini mwanzo wa mkutano kasha wanaendelea na shughuli zao na kuacha kuhudhuria vikao vingine ambapo vinawataka wao kushiriki ipasavyo.

Kupungua kwa mwamko na hamasa ya ushiriki inaweza pia kuwa miongoni mwa sababu inayoendana na kuzoea bunge. Kwani inawezekana katika vikao vya awali wengi wa wawakilishi wetu katika kikao cha maamuzi walikuwa na upya ambao ilikuwa chachu ya ushiriki kikamilifu jukumu lao la kuwepo kikaoni kwa niaba ya wananchi wote wa jimbo wanaloliwakilisha.

Nachelea kuamini kuwa kupungua kwa mwamko na hamasa kumeanza kwa wawakilishi wetu ambako kunawafanya wasihudhurie kwani endapo ndivyo basi ile hali ya “business as usual” (mambo kama kawaida) itakuwa tayari imetamalaki ambayo inachagiza ufanywaji wa mambo bora iende kukamilisha muda na si kuzingatia ufanisi, tija na viwango kwa maslahi ya wananchi waliowatuma kuwawakilisha na Taifa zima kwa ujumla wake.

Lakini katika kujaribu kuendeleza tafakuri juu ya nini hasa ambacho kinaweza kuwa kinawasibu wawakilishi wetu, maana nafahamu spika na waratibu wa bunge hawawezi kugonganisha ratiba za bunge na kazi za kamati au majukumu mengine ya kibunge kiasi cha kufanya ukosefu wa ushiriki mkubwa kiasi kile katika vikao mathalani hiki kikao kinachoendelea cha bajeti. Inawezekana kule kuchanganya siasa na biashara kukawa pia moja ya sababu ambazo zinawafanya wabunge wetu kutokutulia bungeni kwani kwa baadhi ya wafanyabiashara ambao wao ndio wahusika wakuu katika utendaji inaweza kuathiri sana ushiriki kikamilifu wa vikao vya kibunge.

Kwani kama ni shughuli ya kijimbo, naamini wananchi wote wanafahamu na kuelewa kuwa mwakilishi wao wamemtuma bungeni katika kikao kuwawakilisha hivyo kama ni wananchi makini wenye kujua haki na misingi yao ya kiuraia wanapaswa wamhoji wanapomuona mwakilishi wao akiwa jimboni wakati shughuli za kikao cha bunge zikiendelea.

Umuhimu wa kuwepo wa makatibu wa wabunge na watendaji wengine wa ofisi za mbunge ndipo unajitokeza hususan katika vipindi vya vikao bungeni, endapo mbunge anakuwa makini kuhakikisha anakuwa na wasaidizi wataalamu na watendaji kama makatibu wa mbunge ni watumishi imara kuweza kuendelea kuwahudumia wananchi katika kipindi ambacho mbunge anakuwa katika kuhudhuria vikao vya bunge.

Hakika kama wananchi ambao tunawakilishwa na wabunge wetu, ni muhimu kuhoji nini hasa kinachowafanya wawakilishi wetu kutokuhudhuria vikao vya bunge ambayo hasa ndilo jukumu na kazi ambayo walipia kuomba tuwapatie.

Achilia mbali wale wabunge ambao tayari tumeanza kuonyeshwa kupitia vyombo vya habari kuwa licha ya kuhudhuria kwao katika vikao wanakuwa wao kama hawapo kwani wanaangukia kuuchapa usingizi au wakipiga soga wakati mijadala ikiendelea.

Na hivi tunashukuru sana wananchi kupata fursa ya kufatilia vikao vya bunge kupitia vyombo vya habari kama televisheni, je visinge kuwapo hali ingelikuwaje?

Baruapepe: michael@michaeldalali.com

© Michael Dalali, Julai 2011

No comments: