ADVERT

30 August, 2010

Tunawaona,Tukashtaki kwa nani?

Na Michael Dalali

“Watu wameanza kampeni”, “wanagawa fedha na zawadi mbalimbali” ni baadhi ya kauli ambazo zimeshaanza kusikika toka kwa wananchi wengi mahala pengi. Si kauli za kupuuzwa!

Magazeti kadhaa yameripoti shutuma za baadhi ya wananchi wenye nia ya kugombea uongozi ngazi mbalimbali kuanza kampeni za chini chini zisizo rasmi. Nyingi zimeachwa kama tuhuma, nani wa kufatilia?nani wa kusaidia kuthibitisha?

Ni kawaida katika nchi yenye kusimamia uwepo wa demokrasia kuweka jitihada za dhati kuwa na chaguzi huru na haki. Uwepo wa usawa katika kinyang’anyiro kizima cha kugombea ni moja ya tunu kwa chaguzi huru na haki. Je tunu hii inalindwa kwa kiasi cha kutosha?

Wananchi ni nguzo madhubuti kuhakikisha usawa na haki vinastawi katika chaguzi zetu. Watu ndiyo waundao mfumo mzima katika jamii. Nguvu ya umma si ya kupuuzwa!

Mifumo iliyopo chini ya taasisi zinazosimamia na kuchochea demokrasia ni sehemu tu nchini ambayo wananchi wakishiriki vyema wanauwezo wa kuleta mabadiliko!

Je waripoti wapi kwa namna gani?na je vipi hatima ya usalama wao? Fursa zilizopo chini ya taasisi mathalani msajili wa vyama, tume ya taifa ya uchaguzi, vyama vya siasa, asasi za kiraia, vyombo vya habari, zinahitaji sana nguvu ya wananchi ambao ni mashuhuda wa kila matukio yanayotokea kila kukicha katika maeneo yao. Huku ndiko mahala pakushtaki!Twende Tukashtaki!

Sheria zinazosimamia mchakato mzima wa chaguzi mathalani matumizi ya fedha katika kampeni inaweka wazi uzito wa vitendo na kuweka bayana adhabu ama hatua zitakazochukuliwa kwa aina ya mgombea, au chama kitakachopatikana hatia.Kwanini baadhi wanajifanyia mambo kana kwamba hakuna sheria wala taratibu? Kazi kwetu!

Mara nyingi wananchi hufurahia na kulea vitendo kama kusafirishwa toka mahala fulani kwenda mkutanoni na kurudi ama kukodishiwa pango ama mahala pa kulala na watu wenye nia ya kugombea nyadhifa mbalimbali.Wakijilinda kwaa fikra ya kula chako mapema. Je kweli tunataka mabadiliko?

Jenerali Ulimwengu aliwahi sema; “hakuna ukarimu unaozuka ghafla katika mwaka wa uchaguzi hata mtu akajikuta anatoa zawadi za mamilioni ya shilingi wakati katika uhai wake, na akiishi miongoni mwa watu wake hao hao, hajawahi kutoa hata chapa moja kwa “Yalla, maskini”. Huu ukarimu unaokuja kama surua umetoka wapi?”

Vyama vya siasa, asasi za kiraia,vyombo vya habari vitumikapo vyema ni waangalizi wazuri katika kuhakikisha demokrasi inastawi nchini. Tukaripoti huku.

Hebu fikiria namna gani utakuwa umechangia kuboresha demokrasia nchini endapo mtu uliyemripoti ndani ya chama chake ama chama tofauti kukiuka sheria na taratibu za chaguzi nchini akiwekewa pingamizi kutogombea.

Tusisahau, mgombea afanyae vitendo vya kukiuka maadili, taratibu na sheria tulizojiwekea hata kama ni “kiongozi mzuri” kiasi gani hatufai!

Wengi wanawaona wagombea wanaokiuka sheria, taratibu na maadili lakini bado hawajuhi kama wanguvu kubwa kuwadhibiti! Na wanauwezo kuwashtaki!

Aliyewahi kuwa mwanasiasa mweledi na rais wa Ufaransa miaka ya 1959-1969, Charles De Gaulle aliwahi tanabaisha; “nimefikia hitimisho kwamba siasa ni jambo zito sana kuwaachia wanasiasa”!

Kama kweli tunataka kujikwamua katika hali duni ya maisha tuliyopo, ni jukumu la kila mwananchi kuhakikisha uwepo wa siasa safi ambayo italeta usimamizi bora na uongozi bora nchini wenye kujali ustawi wa nchi nzima na maendeleo yanayogusa maisha ya mwananchi mmoja mmoja.

Jukumu la kuleta mabadiliko haya lipo mikononi mwa kila mwanachi. Kwa kila mwananchi kuhakikisha wagombea wote wanafuata kanuni, taratibu na sheria ndiyo njia pekee kujenga uwepo wa siasa safi na madhubuti.

Mabadiliko yanawezekana! Shiriki kikamilifu!

michaeldalali@yahoo.com, 0717-011112

No comments: