ADVERT

04 October, 2008

Falsafa ya “Fundo” la Muwa na Taifa Makini

Falsafa ya “Fundo” la Muwa na Taifa Makini

Na Michael Dalali.

Falsafa kadha wa kadha ni miongoni mwa nadharia madhubuti zitoazo fikra pana kwa jamii huku zikifungua mawanda mapana ya mitazamo ambayo ni muhimu kwa udhabiti wa jamii endelevu.

Licha ya nadharia ya falsafa ya “Fundo” la muwa yalihusu kwa upana Taifa zima lakini kwa kuwekeza nguvu katika rika la Ujana kama rika tete na tegemeo kwa taswira ya Taifa lolote ndipo kiini cha mabadiliko yatajikita na kutoa cheche zisambaazo kama moto katika nyasi kavu kwa makundi yote katika jamii.

Ujana ni moja ya umri ambao hutazamwa kwa umakini sana na jamii makini kwani ni katika kundi hilo taswira na hatima ya Taifa hujengeka.

“Nchi inayoweza kudumu na kuendelea ni ile tu ambayo wananchi [hususan vijana] wake wanatafakari masuala, wanasaili na kujisaili, wanakosoa na kujikosoa, wanabishana kwa dhati. Kila siku wakitafuta kipya kinachoweza kuwaendeleza, wanasaka ujuzi na maarifa bila kupumzika, wanakataa kumezeshwa “kweli” zisizo na msingi wowote. Nchi isiyokuwa na watu wenye sifa hizo si taifa bali ni mkusanyiko wa watu ambao silika yao lazima iamuliwe na watu wengine ambao maslahi yao yanaweza kuwa ni kuwafanya watumwa” Jenerali Ulimwengu.

Katika jamii yetu ya Tanzania vijana ni tunu ambayo licha ya uwezo na umakini wake bado ina changamoto nyingi sana ambazo falsafa ya fundo la muwa inajaribu kuzichambua kuelekea utamu halisi.

Licha ya kelele nyingi sana za vijana katika kudai kushirikishwa bado kuna haja na deni kubwa kwa vijana wenyewe kujidhatiti sana katika kuelekea ushiriki wao wa madhubuti ili hatimaye waweze kula utamu wa muwa.

Ni namna gani vijana wanajiandaa na changamoto za kimaisha ambazo zinakuwa mithili ya fundo katika kuelekea utamu wa rika walilopo? Je jamii inawasaidiaje kuvuka vizingiti wa changamoto hizi mithili ya uwepo wa matumizi ya visu na vifaa kama hivyo katika uvunjwaji wa fundo la muwa?

Vijana wana elimu bora yenye kuweza kuwawezesha kukabiliana na changamoto wa mazingira waliyopo ama wana bora elimu?

Wengi wamekuwa wakikimbilia kufananisha mafanikio ya kitaaluma na upatikanaji wa alama za juu mathalani daraja la kwanza ama “A”, sawa hicho ni kipimo kizuri kimoja wapo lakini hakitakamilika endapo mhusika hataweza kulitafsiri daraja alilolipata ama alama aliyoipata katika matendo hususan kujikwamua na changamoto zake zimkabilizo.

Kwa kumiliki daraja la kwanza ama alama ya juu ambayo huwezi kuitumia na kuidhihirisha hususan katika kukabiliana na changamoto kadha wa kadha katika fani husika ama maisha yako ni sawa na debe tupu!

Lakini hii inatokana sana na namna ambavyo mfumo wetu wa kuelimisha ulivyo. Lakini si mfumo tu, bali hata mhusika jinsi alivyo na anavyojirahisi na kuukubalia mfumo umpeleke ndiko siko!

Hapa ndipo wasomi na wataalamu mathalani Will Durant aliwahi kusema; ufahamu ni nguvu, lakini busara pekee ni uhuru [tafsiri ikiwa yangu] “Knowledge is power, but only wisdom is liberty”!

Naye Marcus Garvey mmoja ya wanaharakati wa kutetea haki za watu weusi aliwahi andika kitabu chake cha Ujumbe kwa Watu “Message to The People” ambapo alitanabaisha umuhimu wa kujiimarisha kwa kutafuta maarifa na thamani yake mathalani kuweza kudhihirisha pundi mhusika anapokuwa na maarifa ama ujuzi fulani anaweza kuwa kama mtawala katika maarifa hayo na kupelekea kushinda washindani wengine nakupelekea kujijengea umahiri na kuaminika.

Mara kwa mara tofauti kubwa sana na hata wakati mwingine hupelekea baadhi kuogopwa katika jamii licha ya udogo ki umri huja kwa uwezo wa ufahamu na kuweza kuhusianisha ufahamu huo na mazingira halisi yamkabiliyo mhusika, hapo ndipo dhana na umuhimu wa maarifa huja.

Hapa ndipo wanaibuka vijana ambao huhitajika sana na wenye soko katikati ya madhila ya ukosefu wa ajira ili tu waweze kuchochea maendeleo ya jamii kwa umadhubuti wao wakuwa wanafikra “Think Tanks”!

Vijana hawa wanaweza kupinga vizingiti kadha wa kadha mathalani vya umri, ujana, kisomo cha wastani wa juu[ingawa si lazima idadi nyingi ya shahada] na kuweza kuosha mikono yao na kustahili kuaminiwa na kutegemewa kama wabobeaji wa fikra “Think Tanks” ambao huweza kutoa mitazamo mipya.

Ikumbukwe si kila msomi ni makini na mwenye uwezo wa kung’amua maono na kuwa mwanafikra “Think Tank!” lakini nchi mathalani Tanzania inaweza kufanya juhudi ya dhati kutengeneza vijana kama hawa wanafikra pana kufaa katika matumizi ya nyanja mbali mbali mathalani taasisi za kiserikali, binafsi, mashirika ya umma, vyama vya kiraia, vyama vya kisiasa.

Kwa kila taasisi makini na madhubuti itajitahidi kuweza kupata wanafikra makini na pana “Think Tanks” kama hawa ili kuelekea ustawi wa taasisi hiyo.

Kwa ustawi wa taasisi tunapaswa kupata vijana wengi sana wenye uwezo wa juu wa kifikra “Think Tanks” ambao wanauwezo wa kuona zaidi ya maono ya kawaida.

Lakini si tu taasisi zetu kuwa na vijana wa kutosha wenye umakini wa kifikra na maono “Think Tanks” bali pia kuwa na taasisi zenye fikra na maono “Think Tank Institutions” hata kuweza kukinzana na hatimaye kupata ulalo mzuri wa hoja ambazo huhitajika katika ujenzi wa jamii makini yenye kuelekea ubora wa ustawi na si taasisi moja kumeza nyingine na kubaki pasi mpizani ama changamoto katika utendaji wake.

Mwalimu Nyerere aliwahi kutanabasisha Taifa kwa ujumla katika kitabu chake cha Tujisahihishe kuwa moja ya makosa ambayo tunapaswa kujisahihisha ni kutojielimisha.Na kuchambua fikra za wengi kuwa mosi; kusoma ni mpaka kujiunga katika vyuo mathalani Vyuo Vikuu ama nje ya nchi. Pili; kufikiri kuwa tunajua kila kitu na hatuna haja ya kujifunza jambo lolote zaidi.”Mwanzo wa elimu ni kutambua kuwa hatujui kitu!”.

Je ni kwa namna gani vijana tunang’amua fursa hiyo na kujiandaa ipasavyo kuweza kuwa wanafikra makini “Think Tanks” wenye kuweza kutoa maono mapya katika nyanja za fani zetu? Ni kwa vipi vijana tunajiandaa kuweza kukabiliana na misukumo ya changamoto za kimaisha mathalani ukosefu wa ajira na kutumia umahiri wa fikra na maono kujinasua katika changamoto hizo?

Na ndiyo maana Hayati Bob Marley aliweza imba tungo ya ukombozi wa kifikra katika Wimbo wa Ukombozi “Redemption Song” ;

“Jikomboe kutoka utumwa wa kiakili,

Hakuna mwingine isipokuwa sisi wenyewe

Tunaoweza kukomboa fikra zetu

Wala msiogope nguvu za kiatomiki

Sababu hakuna hata moja itakayosimamisha muda……..”

“Hakika huwezi kula muwa pasi kula fundo” na “tamu ya muwa yenyewe ni fundo”!

© Michael J. Dalali.


ANGALIZO: Makala hii iliwahi kuchapwa katika gazeti la MWANANCHI mnamo tarehe 30.09.2008 katika kolumu ya Tafakuri Tanduizi....hii ndiyo makala halisi kabla ya maboresho ya wahariri.Shukrani zangu za dhati kwa wahariri na menejimenti ya gazeti la Mwananchi kwa ushirikiano. Na hasa kwa namna ya pekee wana Tafakuri Tanduizi wenyewe "Wanazuoni".mathalani Kamaradi Chambi Chachage kwa kuendeleza harakati.


Aluta Continua!

1 comment:

Anonymous said...

kaka makala imetulia ila jaribu kuweka fupi fupi at least key message.