ADVERT

21 September, 2008

Septemba 20, 2008

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
KUKAMILIKA KWA MUHULA WA KWANZA YA PROGRAMU YA MAFUNZO KWA VIJANA
“SCHOOL OF TYVA”

Ndugu zangu waandishi wa habari,
Awali ya yote napenda kuwashukuru kwa kuitikia mwito wangu wa kuja kuzungumza nanyi. Nasema hivi kwa sababu kwa nguvu zenu hususan katika taaluma yenu hii ya habari na umuhimu wake mkubwa katika kuelekea jamii huru, ahaki, yenye uwakilishi bora mathalani wa vijana kazi ambayo mnajitahidi kila kukicha.

Tanzania Youth Vision Association [TYVA] ama Asasi ya Dira ya Vijana Tanzania ni asasi ya vijana, isiyo ya kiserikali na isiyofungamana na itikadi, kikundi wala chama chochote cha kisiasa. TYVA ilianzishwa mnamo mwaka 2000 na kupata usajili wakitaifa mwaka 2002 kwa hati ya usajili nambari SO.NO. 11454.

Dira yetu: Kuwa na jamii huru, ya haki, ya kidemokrasia na yenye amani ambayo ina ushiriki hai wenye manufaa kwa vijana.

Asasi ya Dira ya Vijana Tanzania [Tanzania Youth Vision Association] kwa kushirikiana na shirika la British Council chini ya Mradi wa Debate to Action “DTA” imeweza kuendesha mafunzo yenye lengo la kujengea uwezo kwa vijana nchini mathalani katika ubunifu na usimamiwaji wa miradi, uongozi ili waweze kuimarisha utekelezaji wa mradi wa Debate to Action hususan katika ngazi ya asasi shiriki.

Programu hiyo ambayo ilipewa jina la “School of TYVA” imeweza kutoa matunda mengi toka kuzinduliwa kwake mnamo Mei 4, 2008 hadi leo hii Septemba 20, 2008 ambapo muhula wa kwanza unamalizika kuruhusu kufanyika kwa tathimini, kuboresha na kupanua programu.

Programu hii imeonesha mafanikio kwa kiasi kikubwa, kwani idadi ya washiriki imezidi kuongezeka maradufu kuanzia vijana nane tulipoanza hadi zaidi ya mia moja leo hii.Umahiri katika kusimamia matukio na kubuni miradi katika ngazi ya asasi pia umeongezeka.Wadau walioonesha nia ya kufanya nao kazi imezidi kuongezeka, ikihusisha asasi za kiraia pamoja na wafadhili mbalimbali.

Ndugu wanahabari, kwa kutambua mchango wenu kwenye maendeleo ya asasi za vijana na taifa kwa ujumla, wito wangu kwenu ni kuwaombeni kufikishia taarifa ya fursa hii adhimu na thabiti kwa vijana wengi zaidi nchini. Hii itaboresha ongezeko la vijana wenye uwezo wa kushiriki kikamilifu katika michakato ya maendeleo.

Nikirudi kwa wanachama na vijana kwa ujumla, niwakumbushe kilomita moja huanza na hatua moja. Pamoja na nia thabiti, fursa tunazozipata, na uwezo tunaojijengea ndiyo nguzo muhimu katika kuwa wadau wakuu katika michakato ya maendeleo.

Kwa kuhitimisha, programmu hii ya School of TYVA kama ilivyoalezwa kabla imekamilisha muhula wake wa kwanza leo tarehe 20 Septemba 2008 kutoa fursa ya kutathmini tulipotoka, tulipo, na tunapoelekea. Hiyo itashirikisha kamati kuu ya programu, asasi kwa ujumla na wadau wachache wenye nia ya kusaidia na kufanya nao kazi. Taarifa zaidi zitatolewa kwa umma, pindi tathmini itakapokamilika.

TYVA imejitolea kwa dhati kukuza uwezeshaji na kujing’amua kwa vijana kwa kuwa na programu fahamu, zenye kujenga uwezo na mitandao yenye kulenga vijana, yenye kuzingatia jinsia, rafiki kwa mazingira na zipatikanazo kwa ufanisi na kwa vijana walio katika mazingira magumu.

Asanteni Sana Kwa kunisikiliza!
Mungu ibariki Tanzania
Imetayarishwa na;

……………………
Justin M. Rwelengera
Mkuu wa Idara ya Mafunzo na Uwezeshaji
0713-03 99 77

No comments: