Na Michael Dalali.
Siasa ni jambo la ajabu sana ambalo ndilo limekuwa na tafsiri mbalimbali duniani toka kwa wanazuoni wengi toka enzi za Aristotle hadi wanazuoni wa sasa kama kina Prof. Baregu waliojaribu na wanaoendela kila kukicha kutafakari undani wake.
Wasomi wa sayansi ya siasa "political scientist" wanadiriki kujitofautisha wao na wanasiasa "wafanya siasa" kwa minajili ya kujiweka mbali na tamaduni hasa zilizopo katika siasa.
Haya Mwalimu Julius K. Nyerere aliwahi kutuasa kwamba katika moja ya nguzo kuu ya maendeleo ambayo tunayatafuta yanaweza kufikia endapo tutapanda na kudumisha siasa safi katika nchi yetu.
Hii ni kutokana na uwepo wa dhana kali sana ya "siasa ni mchezo mchafu" ambayo huleta maafa na hasara kuwa sana katika uendeshwaji mzima kwani huweza kumuingiza madarakani mgombea si kwa sifa bali uwezo wake madhubuti wa kuucheza mchezo mchafu.
Lakini wapo waliofikia kutoka kauli ambazo zimekuwa kama nguzo za tafakari kutokana na namna ya uchafu na uendeshwaji wa siasa hasa katika vipindi kama vya kampeni na uchaguzi tayari kushindania kunyakuwa madaraka.
Mgombea Ubunge katika uchaguzi wa mwaka 2005 jimbo la ubungo aliye mwagwa na mkongwe aliyekuwa waziri wa awamu ya tatu wa Chakula na Kilimo Mhe. Charles Keenja[CCM], ndugu John Mnyika[CHADEMA] aliwahi kutoa kauli ambayo ndiyo kiini cha tafakari dhidi ya yanayoendelea katika heka heka za uchaguzi mdogo wa Kiteto.
Ndugu Mnyika alisema "Siasa si Uadui" naamini alikuwa akimaanisha kuna haja ya kufanya siasa bila kujengeana chuki, hasira, hujuma na hata kudhuliana kwani siasa si uadui ni juu ya kutafuta ridhaa ya wananchi uwatumikie.
Wapo waliodhidi kusema madaraka yapatikanayo yanapaswa yatoke kwa watu kwani sauti ya watu ni sauti ya MUNGU hivyo hakuna haja kuwepo na siasa chafu.
Naamini si asilimia kubwa sana ya wananchi wa Tanzania kwa sasa wapo makini sana kufatilia kinyang'anyiro cha siasa kinachoendelea huko katika jimbo la uchaguzi la Kiteto lililoachwa wazi kutokana na kuaga dunia kwa Mbunge Benedict Lusulutya[CCM].
Hii inatokana na kugubikwa kwa matukio mazito sana ya kitaifa ndani ya kipindi hiki cha muda wa kampeni ya uchaguzi wa Kiteto.
Kusomwa kwa ripoti ya tume ya Mwakyembe juu ya Richmond kitu ambacho kilizaa kujiuzulu kwa Kiongozi wa juu wa serikali bungeni, aliyekuwa waziri mkuu Mhe. Edward Lowasa[CCM] na mawaziri wawili Nazir Karamagi na Msabaha wote wakituhumiwa kuhusika katika sakata hilo.
Kuvunjwa kwa baraza la mawaziri kitu ambacho watanzania walikuwa wakikisubiri kwa hamu sana na kilifuata kutokana na muongozo wa Katiba kisheria.
Kuteuliwa Waziri Mkuu mpya Mhe. Mizengo Pinda na baada ya muda baraza zima jipya la mawaziri lenye sura mpya mbalimbali za watendaji na pia kupunguzwa idadi ambayo haikuwa ya lazima kwani ilizaa mzigo mzito wa serikali.
Uwepo wa ziara ya kipekee pale Tanzania ilipompokea Raisi wa Marekani na kukaa nae takribani siku nne akijionea uzuri wa Tanzania na mali asili zake mbichi zinazowatoa udenda wawekezaji [wa ndani na wa nje] na kupata fursa ya kukagua miradi kadha wa kadha inayofadhiliwa na serikali yake.
Hivyo juu ya baadhi ya matukio vinara kama hayo yaliweza kuteka medani ya habari nchini na fikra za wananchi wengi sana hata kutoweza kufatilia kwa umakini na undani habari kama za uchaguzi wa Kiteto.
Ipo habari iliyopamba vyombo vya habari juu ya kupewa kitu cha kudhuru kinachosadikiwa kuwa na sumu mgombea ubunge wa tiketi ya upinzani ndugu Kimesera Victor kitu ambacho kilipelekea kukimbizwa jijini Dar-Es-Salaam kwa matibabu ya zaidi hatimaye akarejea na afya tayari kuendeleza kampeni.
Wapo waliochukulia kama hujuma toka Chama Cha Mapinduzi dhidi ya mgombea wa upinzani huyo ambaye anasemekana kukubalika na wananchi wake ili kujaribu kumuondoa duniani.Allahmdulilah haikufikia huko!
Lakini wiki hii tena kuwepo kwa tukio la shambulio tena ndani ya ofisi za chama cha CHADEMA na kuwajeruhi baadhi ya viongozi wa juu wa chama wanaoshiriki kampeni na kumjeruhi vibaya kwa kisu dereva wa gari la chama hicho ndugu Daudi Baraka ni habari ambazo si za kuziacha bila uchambuzi wa kina.
Haya yananikumbusha shambulio la wanahabari ndani ya ofisi zao wakiwa wanaandaa habari za gazeti lao la mwanahalisi ndugu Said Kubenea na Mshauri wake Ndimara Tebagambwe kama njia ya kuhujumu nyanja ya usambazaji wa habari za uchambuzi wa kina dhidi ya yanayojiri kila kukicha hasa katika utawala na tabaka la viongozi dhidi ya maslahi ya taifa zima.
Kujeruhiwa kwa Hamadi Mussa Yusuph-Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Zanzibar, Juju Danda-Afisa mwandamizi kurugenzi ya bunge na halmashauri kuu Taifa, Joseph Freme-Mwenyekiti wa Chadema Ruvuma na mjumbe wa kamati kuu, Msafiri Mtemelwa-Kaimu Mkurugenzi wa Kampeni na Uchaguzi na Selemani Mohamed-Mjumbe wa uchaguzi Kiteto ni swali zito la aina ya siasa inayoendeshwa hapa nchini.
Siasa za kutumiana vikundi vya vijana kufanyiana vurugu kama walivyotumiwa viongozi hao kundi la Green Guard toka Dar-es-Salaam kuwavamia wakiwa ofisini kata ya Kijungu, kweli hiyo ndiyo demokrasia ya kweli?
Chombo cha Umma nacho kukiuka maadili kwa kuwapiga wanasiasa hao waliofikishwa kituo cha polisi, hata kuwacheleweshea muda wa kupata matibabu na kuwaongezea maumivu.
Lakini vilevile wanasiasa wa Chadema nao wanaolalamikiwa kupiga kelele kwa kusimamia kwaya kitu ambacho kinabugudhi shughuli za wengine, je ni ukomavu wa kisiasa?
Wakati wananchi wa Kiteto wakielekea kupiga kura mnamo tarehe 24.02.2008 tayari kufidia pengo lililoachwa wazi. Ni bora kutoweka mbele woga wala kuribuniwa na ahadi za uwongo, wanapaswa watafakari ni sera zipi ndizo zinawafaa kuwaongoza na kuamua pasi shindikizo la aina yoyote.Na tukumbuke Siasa si Uadui!
Mungu Ibariki Tanzania, Mungu Ibariki Kiteto.
0755-45 97 83
michaeldalali@yahoo.com
No comments:
Post a Comment