Nipo ndani ya boti tayari katika msafara kuelekea Tanzania Visiwani, visiwa maarufu kwa marashi ya karafuu.Zanzibar kwenye historia inayojidhihirisha kila kona upitayo kitu ambacho kinajenga kivutio kikubwa katika utalii.
Kisiwa hiki chenye kupokea wageni wengi sana hasa katika misimu ya kitalii huweza kutangaza utamaduni na historia ya kiafrika iliyopo katika sehemu hasa kama maeneo ya mji mkongwe wa mawe “Stone Town”.
Kila binadamu anajengeka vyema akichangiwa na utamaduni mahalia ambao huchanganya vitu kama lugha, mavazi, taratibu, sheria, vyakula, nyimbo, michezo, imani[wakati mwingine kupitia dini] n.k.
Kuna matamasha mengi huwa yanatayarishwa mara kwa mara kila kona ya nchi kuwa vuta makundi ya rika mbali mbali lakini si yote huweza kufanikiwa kuwakutanisha watu wa rika tofauti na nchi mbalimbali na kuweka usawa hasa katika kulinda na kukuza tamaduni kupitia matamasha hayo.
Kivutio kimoja wapo kikubwa katika matamasha nchini hasa yanayofanyika Zanzibar kwa sasa huwezi kukosa kilitaja tamasha la “Sauti za Busara” ingawa yapo mengine mengi pia kama “Film Festival”.
Kama jina la tamasha linatoa mchango mkubwa sana katika kukuza busara kwa wahudhuriaji hasa wenye umakini wa kufatilia mistari inayoimbwa na wasanii mbalimbali toka kona na pembe za dunia.
Huu ni upekee kwa tamasha kukutanisha wasanii toka mataifa mbalimbali katika kazi moja ya sanaa ya jukwaani ya muziki, kiwasilisha ujumbe.
Lakini vilevile tofauti na usemi wa kiswahili wa “mafahari wawili hawakai katika zizi moja” katika tamasha la sauti za busara huweza kuwaweka mafahari wa muziki toka pembe mbalimbali za dunia tena wenye kuimba ladha tofauti za muziki kwenye jukwaa moja.
Hapa unaweza kushangaa sana lakini ndivyo ilivyo unapata ladha ya taarab na baada ya muda unapokea ladha ya HipHop na kufuatuatia na ladha nyingine kadha wa kadha.
Ndani ya Ngome Kongwe huweza kuzizima sauti za vijana na wazee wanaopata burudani ya tamaduni mbalimbali huku wakijikumbushia historia yao kama juu ya utumwa, utawala wa kisultani, ubaguzi wa rangi[ingawa bado unaendelea].
Kwani ni katika jumba la Ngome Kongwe ndipo likikuwa kama kiini cha ulinzi dhidi ya maadui miaka ya nyuma wakati wa milki ya kisultani ndani ya Zanzibar.
Lakini ni busara kuweza kutoa nafasi kwa wananchi wa visiwa kuweza kuzalisha mali kwa kupitia utalii na sanaa kwa tamasha hili kuwaleta watalii wengi na kuwakusanya.
Ndani ya jumba la Ngome Kongwe wananchi toka sehemu mbalimbali za Tanzania wanapata fursa ya kutumia neema inayoletwa na tamasha kutangaza, kutambulisha na kuuza kazi mbalimbali za kisanii zaidi ya nyimbo kama picha na michoro mbalimbali ya kiusanii inayovutia, vinyago vyenye ujumbe wa kipekee, kazi za aina nyingi za sanaa ya mikono hupatikana.
Vilevile kwa wasanii makini wanatumia mwanya wa tamasha kama la sauti za busara kuweza kuuza moja kwa moja kazi zao za kisanii kama kaseti "tape" na "cd" zao hivyo kudsaidia kujikinga angalau na lindi la unyonyaji wa kimauzo kwa kazi zao dhidi ya wasambazaji.
Kuna fursa ya matamasha kama haya kuweza kutumika vyema kupenyeza ujumbe mbalimbali makini na wa kibusara kwa kundi rika la ujana.Mathalani juu ya mapambano dhidi ya ugonjwa wa UKIMWI ama umuhimu wa uwajibikaji katika kujenga taifa kwa kila mmoja kutimiza wajibu vyema kama ipasavyo.
Vilevile mapato yatokanayo na tamasha pia yanaweza kwa asilimia fulani kutolewa kwa kutatua moja ya shida za kijamii hasa katika eneo husika.Mfano: sehemu ya mapato yakitolewa katika uboreshaji na utunzaji wa jumba la Ngome Kongwe kama mchango kwa jamii.
Hiki ni moja wapo cha nyenzo bora ya utangazaji wa utalii ndani ya nchi yetu.Waandaaji wameweza kutumia busara hata kwenda sambamba na mabadiliko ya haraka ya kiteknolojia kwa kuweza kufungua tovuti [www.busaramusic.org] na kuwafikia watu wengi kila kona ya dunia na kuwahabarisha juu ya tamasha la mandhari adimu ya visiwa vya Zanzibar.
Katika utalii hapa ikumbukwe hata utalii wa ndani ya nchi yaani wananchi kutembelea sehemu mbalimbali za kitalii ili iwawezeshe kujifunza na hata kupumzika baada ya mihangaiko na mikiki mikiki ya maisha ya kila siku.
Utamaduni ambao kundi kubwa la wazalendo wa Tanzania hawana.Kwa hapa ifahamike utalii si ishara ya utajiri bali ni utamaduni ambao tunapaswa kujijengea hata kwa wenye kipato kidogo.
Lakini vilevile hata unafuu katika gharama za viingilio vinavutia sana kuona kuna uhitaji wa ujumbe ufike kwa watu wengi hivyo kwa kuwepo na viingilio vinavyowezwa na vijana wengi wanaweza kuwafikia kundi kubwa la vijana.
Shime uwepo wa matamasha mahiri na yenye ubora katika tanzu mbalimbali za sanaa, tayari kwa kukuza mila na tamaduni halisi za kitanzania na si kuwa chachu ya mmomonyoko wa maadili ya kitanzania.
No comments:
Post a Comment