ADVERT

20 February, 2008

Jicho la Mnyika juu ya JAMBOFORUMS!

Wednesday, February 20, 2008

Kwa niaba ya Baraza la Vijana wa CHADEMA(BAVICHA), vijana wa CHADEMA tunaungana na wapenda uhuru, haki na ukweli kote nchini kulaani uamuzi wa Jeshi la Polisi kuwakamata na kuwaweka ndani vijana wa wawili wa kitanzania Maxence Melo na Mike Mushi kwa sababu ya masuala ya mtandao wa Jambo Forum(www.jamboforums.com).

Uamuzi wa kuwakamata na kuwaweka ndani kwa takribani saa 24 na kuwahoji kwa zaidi ya saa 14(usiku na mchana) tunaona ni kinyume cha sheria ambayo inaeleza bayana mtuhumiwa anapaswa kuhojiwa si zaidi ya masaa manne kwa mfululizo na kwa ujumla ni uvunjaji wa haki za binadamu na haki za kikatiba za kupata na kutoa taarifa/habari. Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali katika Jeshi la Polisi, vijana hawa wamekamatwa kwa kutuhumiwa kuendesha mtandao wa Jambo Forum ambao unadaiwa kuwachafua watu mbalimbali ambao vyanzo hivyo vya polisi mpaka sasa havijawataja.

Vyanzo mbambali vya polisi vimeeleza kuwa uamuzi wa kuwakamata vijana hawa umetokana na jeshi la polisi kupata mashtaka toka kwa watu wasiotajwa kwamba mtandao huo umekuwa ukiwachafua watu mbalimbali hususani viongozi wa serikali; suala hili nao linakwenda kinyume cha misingi ya kikatiba na kisheria. Sisi tunaamini kwamba kama kuna mtanzania yoyote ambaye anadhani amekashifiwa na mtandao huo ana haki ya kukanusha ama kuchukua hatua za kisheria kwa kwenda mahakamani. Mikakati hii ya kuzuia uhuru wa habari iliwahi kujitokeza siku za usoni pale upinzani ulipotoa ‘orodha ya mafisadi’ na baadhi ya vyombo vya habari kuchapa majina hayo vilipewa vitisho mbalimbali na watuhumiwa hao wa ufisadi ambao walisema wamechafuliwa.

Serikali na vyombo vya dola ni vyema vikafahamu kwamba uhuru wa maoni kupitia katika mitandao unafaida zake na hasara zake, hivyo kuundoa uhuru wote kwa sababu za malalamiko ya watu wachache, masuala binafsi au migogoro ya familia Fulani ni kuukosesha umma faida ambazo zinatokana na mitandao kama Jambo Forum. Pia serikali ifahamu kwamba sheria nyingi za Tanzania zinasimamia masuala ya habari ziko kimya kuhusu masuala ya habari katika mitandao hivyo, mitandao kama Jambo Forum inalindwa kwa kanuni na mikataba ya kimataifa ambapo imesajiliwa.

Tunarudia tena kukumbusha kuwa mwanahabari ni mjumbe tu wakufikisha ujumbe katika jamii; ambaye anapaswa kulindwa na kuheshimiwa. Tabia inayoanza kuchipua ya kuwanyanyasa wajumbe au chombo kilichofikisha ujumbe tena kwa njia ambazo ni kinyume cha sheria na haki binadamu badala ya kuushughulikia ujumbe wenyewe; ikiachwa ikashamiri inaweza ikatishia ufanisi wa sekta ya habari ambayo inapaswa kudumishwa kama mhimili wa nne wa dola.

Aidha vijana wa CHADEMA tumesikitishwa na kutoweka hewani kwa mtandao wa Jambo Forum ambako kutokana na vyanzo mbalimbali inaelezwa kwamba waratibu wa mtandao huo wameshinikizwa kuufunga kutokana na shinikizo la ‘kigogo’ mmoja wa jeshi la polisi kwa maelekezo toka serikalini.

Jambo Forum Wanahabari imekuwa mstari wa mbele kwa uwazi bila woga katika mapambano dhidi ya ufisadi na kutetea rasilimali za taifa, na kuwa sehemu ya jukwaa la sauti umma kusikika na habari kusambaa ndani na nje ya Tanzania kutia teknolojia ya habari na mawasiliano(TEKNOHAMA). Jambo Forum imekuwa mstari mbele katika kuandika tuhuma za ufisadi na/au matumizi mabaya ya madaraka zinazowakabili viongozi kadhaa wa serikali, makampuni na taasisi mbalimbali.

Mtandao wa Jambo Forums ni moja katika ya vyombo vya habari na majukwaa ya umma yaliyohusika kwa kiasi kikubwa kwa kulifunua na kuliweka wazi sakata la Richmond hasa baada ya kuweka hadharani mkataba wa Richmond na kuchambua mambo mbalimbali yanayohusiana na mkataba huo. Kashfa ya Richmond ndiyo iliyosababisha kujiuzulu kwa Waziri Mkuu Mhe. Edward Lowassa na baadaye kuvunjwa kwa baraza la Mawaziri. Jambo Forum imewezesha ‘siri’ za ufisadi zinazofichwa na baadhi ya vigogo ikiwemo serikalini kuwekwa wazi kwa umma na watumishi mbalimbali wa serikali na taasisi mbalimbali bila majina yao kujulikana.

Mtandao wa Jambo Forum umekuwa ni changamoto kwa mitandao mingine ya serikali ikiwemo kitengo cha mawasiliano cha Ikulu kuboresha ufanisi wao katika kutumia TEKNOHAMA katika kuwasiliana kwa umma. Mtandao huo umekuwa ni ukumbi pia wa vyombo vya ulinzi na usalama ikiwemo polisi kupata mawazo mbalimbali ya umma kuhusu masuala ya uhalifu yanayopaswa kufuatiliwa.

“Inashangaza badala ya serikali kutoa ushirikiano kwa mitandao kama hii inakuwa mstari wa mbele kuona kwamba inafungwa. Huku ni kukinzana na dhamira ya Rais Kikwete ya kuongeza uhuru wa habari na haki ya Taarifa hapa nchini. Sisi tulitegemea vipaji vya vijana wanaotengeneza mitandao mbalimbali vikuzwe kwa maslahi ya Taifa badala ya kukamatwa”.

Vijana wa CHADEMA tunatoa rai kwa umma kutochukulia suala hili kuwa ni tukio dogo linalowahusu vijana wawili waliokamatwa bali litazamwe kama tukio linalohusu maslahi ya taifa, uhuru wa vyombo vya habari na haki za kikatiba za kupata na kutoa taarifa/mawazo.

Hivyo tunaitaka serikali kutoa tamko la kina lenye kueleza ni kwa sababu zipi zilizopelekea kukamatwa na vijana hawa na walalamikaji ni wakina nani. Pia serikali itoe tamko rasmi kama imeufungia mtandao wa Jambo Forum au la na tunawataka watanzania wanaoratibu mtandao huo kwa mapenzi mema ya nchi yao waurudishe mtandao huo hewani mapema iwezakanavyo wakati tamko la serikali linasubiriwa. Kadhalika tunatoa rai kwa yoyote ambae anadhani hajatendewa haki ama amechafuliwa na Jambo Forum ajitokeze kukanusha au kuchukua hatua za kisheria dhidi ya mtandao huo badala ya kulitumia jeshi la polisi ama baadhi ya watu kuhujumu haki ya umma ya kupata na kutoa taarifa.

Katika mataifa mbalimbali duniani, mitandao kama Jambo Forum inachukuliwa kama sehemu ya vyombo vya habari na mahali pa umma kukutana kujadili masuala mbalimbali. Hivyo uamuzi wa kufungia Jambo Forum, ni sawa na uamuzi wa kufungia chombo kingine cha habari kama redio, televisheni na magazeti. Kadhalika, uamuzi wa kufungia Jambo Forum ambapo umma wa watanzania kwa maelfu umekuwa ukikutana kujadili masuala mbalimbali ni sawa na kupiga marufuku kukusanyika huko ambapo ni kinyume cha katiba ya nchi na mikataba ya kimataifa ya haki za binadamu. Mwisho, tunaitaka serikali na vyombo vya dola visidhani Jambo Forum ni Maxence Melo ama Mike Mushi bali mihimili ya Jambo Forums kwani ni umma wa wachangiaji na wasomaji waliosambaa hapa nchini na nchi mbalimbali ambao baadhi yao wanaweza kukamatwa, majukwaa yao kuweza kushambuliwa, lakini mawazo yao ya mabadiliko yataishi milele hata pale ndoto ya maendeleo, uhuru na umoja itakapotimia katika taifa letu.


Imetolewa tarehe 20 Februari 2008 na:


John Mnyika
Mkurugenzi wa Vijana
0754694553

No comments: