Bado wanawake na chozi zito!
Na Michael J. Dalali
Kuna kauli nyingi huwa zinaelezea umuhimu wa wanawake ama mama zetu, wapo wanaosema “nani kama mama”, “ maendeleo ya jamii yanatazamwa kwa mwanamke” “kila mafanikio ya mwanaume nyuma kuna mwanamke” na kauli nyingine nyingi sana.
Naandika makala hii kwa unyenyekevu na uangalifu sana nisije kutafsiriwa myanyasaji wa jinsia, lakini nikiwa na msukumo wa hali ya juu toka ndani kwa vile nilivyokuwa naviona mara kwa mara vikiwakabili wakina mama.
Kwa kweli wao ndiyo chimbuko la asilimia kubwa ya watu maarufu na wakuheshimika kwa jinsi walivyoweza kuwaunda “shape” kimaadili na mienendo. Mifano ni mingi katika hili kama Mwl. Nyerere jinsi alivyokuwa na ukaribu na mama yake, Mwanaharakati Martin Luther King Jr wa Marekani na wengine wengi.
Katika Afrika wanawake wamekuwa wakikabiliwa na changamoto nyingi sana katika maisha yao kwa ujumla. Baadhi ya changamoto hizo ni za kiasili na nyingine huibuka toka katika makundi yawazungukayo mathalani wanaume.
Wengi wanamtazamo kwamba wanawake ni viumbe dhaifu, lakini kihalisia si kama wanavyodhani ndiyo maana hata mwanamuziki wa kimarekani Shaggy aliwahi kuelezea nguvu walizonazo wanawake katika kibao chake “strength of a woman” ama Eva na Delila katika vitabu vya dini.
Si huyo tu hata Ambwene Yesaya “A.Y” mwanamuziki wa kizazi kipya aliwahi kutanabaisha harakati za wanawake katika wimbo wake “mademu watafutaji”. Wapo pia wengine wengi kwa kutumia nyanja mbalimbali wameweza kudhihirisha nguvu, umuhimu na kubainisha hali ngumu iwakabilio wanawake.
Katika sehemu nyingi ndiyo washikiliao koo na familia.Huwa na upendo usioweza kupimika licha ya kuwepo wachache wenye kuwa na mapungufu.
Wengi wanazidi kujishughulisha katika nyanja mbalimbali kuzalisha kipato si kujinufaisha nafsi bali kuinua familia na kukidhi mahitaji. Katika hili wanaume asilimia kubwa huibua mzozo kubwa sana kwa kutokuwa tayari kuwaruhusu washiriki katika shughuli za uzalishaji mali.
Wanawake wakijishughulisha katika kazi za kilimo mashambani huko vijijini huwa ni sawa machoni pa wanaume lakini si kuingilia baadhi ya shughuli mathalani biashara, hofu i wapi? Je si moja ya shughuli za kuzalisha mali?
Wapo waliowahi kutishiwa kuachwa kisa hawatakiwi kujishughulisha na shughuli ya aina fulani.Lakini sijawahi kusikia mwanamke anamchagulia kazi ama kumdhibiti mwanaume katika aina ya shughuli ya kuzalisha mali.
Wapo wanaoamua waingie nao katika shughuli za kuzalisha mali baada ya kuona manyanyaso yanazidi kutokana na kuwa tegemezi kwa mwanaume mzalishaji pekee.Lakini pia ni busara na wanawake kupewa ruhusa kufanya kazi kwani kazi ni kipimo cha utu hata vitabu vya dini vinasema asiye fanya kazi na asile.
Wanaoweza kuweka uso gume gume huingia na kuanza kupambana na mifumo hasi dhidi yao katika nyanja mbalimbali ya kazi.Wapo ambao hususiwa bidhaa kisa wao ni wanawake ati hawapaswi kununuzwa biashara zao na wanaamua kununua za wanaume tu!
Nipo njiani natoka Arusha Mahakama ya kimataifa ya mauaji ya Rwanda kushuhudia mwanamama akimtolea ushahidi wa kumtetea mumewe “Augusto
“ anayehusishwa na mauaji hayo.Ni mwanamke hapa ndiye anayetoa uokoaji huku akiweka pembeni makandamizo yote ambayo labda alikuwa yanamkabili toka kwa mumewe huyo.
Njiani nakutana na wakina mama ambao hata sikupanga kununua bidhaa lakini nashawishika kununua kuwaunga mkono jitihada zao kwani kuna mahitaji mengi yanawakabili.Wapo mchana barabarani jua likiwachoma wakisaka fedha. Kazi za nyumbani zikiwasuburi, shamba la nyanya wanazouza nalo linawangojea maskini wakina mama.
Licha ya hali ngumu mwanaume bila hata huruma anapekua na kuchukua na wakati mwingine hata kumnyang’anya kile kidogo alichoweza kukipata kwa siku hiyo [wakati mwingine hata kama yeye anaajira inayompatia kipato], mara nyingine hata kutoangalia mtaji wa shughuli yenyewe!Mungu wangu,ni uchungu ulioje.
Badala hata ya kufanyia maendeleo fedha anyang’anyayo huishia kuipeleka kwenye ulevi na kurejea nyumbani akiwa bwii chakari na kuanza kumpiga huku akimteremshia matusi kedekede.
Wengine wanadiriki hata fedha hiyo hiyo kwenda kutafuta wanawake wa kuwastarehesha pasi kuangalia familia aliyoiacha hohe hae nyumbani ikikabiliwa na majukumu ya mahitaji lukuki.
Mwanamke wa kiafrika anapambana na hali kama hii kwa uvumilivu na upendo, anaendelea kujitahidi kila kikicha kuiinua familia kwa kujishughulisha ili kutimiza hamu ya kuiona familia katika hali ya maendeleo bila kuikimbia kama wanaume wengi wafanyavyo mambo yakiwa magumu.
Naendelea mbele zaidi nakutana na wakina mama wakikata mkonge maeneo ya mazinde na mkomazi hapa fikra zinazidi juu ya mapambano ya kundi la kina mama kwa maendeleo hasa ya familia na hususan watoto wao.
Ni kazi ambayo imezoeleka kufanywa na wanaume, lakini hivi sana katika kusaka fedha wamekuwa wakiifanya kama vile katika miji wanawake wanaojishughulisha na kubeba zege katika majengo yanayojenga na kushusha injini katika magereji ya magari.
Hakuna wasaa wa vicheko kwa wenye kukabiliwa na matatizo yawahitajio kuyatatua wenyewe, hakuna wasaa wa kukaa mguu juu kumsubiri mume ajere n mahitaji eti kupaka rangi ama hina, thubutu!.Wote wanachakarika katika kusaka noti.
Wapo wanaoendesha shughuli katika mazingira ya joto na kelele kali huku wakipewa fedha kichele na wamiliki viwandani lakini yote katika kuinua familia.Hapa nakumbuka katika miaka ya vita kuu ya pili ya dunia 1939-1945 wanawake walivyokuwa na mchango kushikilia uzalishaji mali viwandani wakati vita ikiendelea.Walipewa nafasi kwa nini katika baadhi ya nyanja kunaingia mizengwe hivi sasa?
Wapo ambao wanadiriki hadi kutoa thamani ya miili yao na utu wao kusudi waweze kupata fedha za kukimu maisha yao na ya watoto ambao baba zao walishawakana kutowajua.Wengi tunawadharau pasi kuangalia undani wa kiini cha tatizo lililowapelekea kufikia pale.
Wapo ambao hujishughulisha na shughuli ya kuuza miili yao kama kimbilio pekee la kikomboa maisha yao kwani wanahitaji fedha za kukimu maisha na hawana ujuzi, mtaji, wala namna waionayo na hujikuta wakitumbukia huko.
Natambua uwepo wa hata kundi la wanafunzi tena wa elimu ya juu ambao hufanya tabia kama hiyo pale fedha zinapowaishia huku wakihitajika kuendelea na mahitaji ya kimaisha na kitaaluma pasi kuwepo mtu wa kutoa huduma hizo, ni hatari!
Kama vile wakina mama wauza nyanya kule barabarani walivyokuwa wanagombea mifuko kuwawekea wateja wao mabasi na magari yakisimama ndivyo baadhi ya wanawake maofisini wanavyogombana na wakati mwingine hata kununiana ili tu kufika ngazi ya juu zaidi na kuweza kupata mapato zaidi kukidhi mahitaji.
Natambua umoja ni nguvu na ushirikiano hujenga,ndivyo ambavyo wakina mama wanapaswa kudumisha licha ya kuwa na kila mmoja haja ya kukidhi shida zinzo mkabili.
Katika nyanja kama siasa huko ndiko kwenye mengi yakutoa chozi. Kina mama wengi wapo wenye uwezo na sifa za kuhodhi nyadhifa mbalimbali lakini si rahisi kama tuonavyo nje pale wachache wanapofanikiwa kunyakuwa nyadhifa kama uwaziri ama viti maalumu bungeni.
Wapo ambao huishia kutumika kama “bigijii” [bubble gum] na utamu ukiisha hutemwa tayari kuingia nyingine.Lakini nao huingia na matarajio na mahitaji yao ambayo wachache sana katika wengi huweza kuyafikia.
Si tu kwenye siasa, hata katika harakati za kujikwamua kwao kupitia nyanja kama ya elimu baadhi wamekuwa wakikumbwa na changamoto cha kuwekewa kauzibe na washika dau mathalani wanaume wakihitaji penzi kilazima wakiwa na kinga ya kung’ang’ania maksi zao na hata wengine kuwafelisha.
Kwa nini baadhi ya wanafunzi wa kike waendelee kutoa vilio kila kukicha kisa kuombwa penzi kilazima na walimu wao? Na baadhi ya wasichana hukumbwa na mimba za utotoni “early pregnancies” na hadi kufukuzwa shule huku mpaji mwalimu akiendeleza tabia yake chafu.
Hawa ni sawa na kina mama ntilie wanaonyang’anywa mitaji yao yote kwa mara moja na mgambo bila huruma kwa kuwanyang’anya masufuria yao ya chakula cha biashara.Hurudi mikono kichwani wakifikiria wapi pa kuanzia na huku watoto wakizidi kulia mahitaji kama njaa, elimu na mavazi achilia mbali wakikabiliwa na maradhi.
Bado kuna mifumo ya kionyonyaji iliyopo chini ya migongo ya riba inayowanyonya sana asilimia kubwa ya kina mama wanaojaribu kuapata mikopo wakiwa na tumini la kujikwamua kimtaji na kuongeza tija kwa uzalishaji bora.
Wanawake wa kiafrika wanaendelea kugawanya, kukandamizwa, kunyonywa na kuonewa. Wapo watetezi wachache tofauti na hitaji halisi. Kuna nyanja nyingi wanapaswa kujikaza na kushiriki kwa umoja tayari kujikomboa na hali duni za kimaisha. Jitihada za dhati za kutafuta maendeleo kila nyanja zisirudishwe nyuma na changamoto nyingi zilizopo.
0755-45 97 83
michaeldalali@yahoo.com
1 comment:
Ya!man naomba sasa habari za februari bila kusahau sakata zima la RICHIMONDI. Mdachi, www.ubehomonga.blogspot.com Pia naomba uwe unaitembelea web yangu ili tuongee kilatini.
Post a Comment