ADVERT

11 February, 2008

"Roho iradhi ila Mwili udhaifu"!

Kuna usemi kwamba siasa ni mchezo mchafu, hii inapelekea fikra na mitazamo mingi sana hasa kwa wananchi juu ya siasa.

Siasa safi ni moja ya nguzo dhabiti zenye kuchochea maendeleo katika nchi yoyote kwani ni kwa kupitia siasa ndipo wanapo patikana viongozi na sera zinazotumika kuongoza nchi hadi kuiletea maendeleo.

Siasa safi pia inachambulia namna ya kufikia kuyapata madaraka kwa njia ya haki na ya uwazi kupitia nguvu ya umma yaani maamuzi ya watu.

Kuna tofauti kubwa kati ya kiongozi na mwanasiasa. Ingawa mwanasiasa anaweza kuwa kiongozi ama pia kiongozi akawa na sifa za kuwa mwanasiasa.Lakini wapo wasio na sifa zote hivyo kumiliki moja ya sifa tu.Hii ni karama toka kwa Mungu, ingawa pia wapo wanaojijenga kwa kupata mafunzo.

Katika moja ya michakato ya kisiasa ni kampeni kipindi ambacho wagombea wa ngazi mbalimbali wanapata fursa ya kujinadi sera zao, nini hasa wanatacho fanya pindi watakapo pewa ridhaa ya kuongoza umma.

Kipindi cha kampeni hugharimu fedha ambazo hutumika katika shughuli mbalimbali mathalani mafuta ya magari kuzunguka maeneo ya wananchi. Wapo ambao pia hugawa vifaa vyenye ujumbe juu ya mgombea kama khanga, fulana, kofia vitu ambavyo huhitaji sana fedha kuweza kuvitengeneza.

Wapo vilevile katika kipindi hiki hupita pita wakigawa fedha kwa wananchi wenye uwezo na hamasa kubwa katika jamii kuweza kuchochea mabadiliko ya kimaamuzi kwa wananchi ili wawe upande wao.

Lakini zaidi wapo wanasiasa ambao katika kipindi cha kampeni huweza kutumia pia fedha kama nyenzo ya kuwadhibiti wapinzani wao katika kinyang'anyiro kwa kuhujumu kila jitihada za mpinzani kwa uwezo wa kifedha. Hapa wapo wenye njia mbalimbali hatari na njia salama.

Kuna makundi mengi sana ya wanasiasa ndani ya medani ya siasa. Hapa wapo wanasiasa matajiri, maskini na wa kati. Wasomi na wasio wasomi. Wenye changamoto za kimwili na wasio nazo, wapo pia wenye kuwakilisha makundi mbalimbali katika jamii kama watetezi wao.Hapa ndipo nguvu za wanasiasa zinapogawanyika.

Nguvu hizi za wanasiasa zinaweza kushuhudiwa katika namna ya utendaji wa kisiasa katika kampeni hata baada ya kampeni. Mfano; uwazi wa namna ya kukusanya fedha na kiwango cha kutumika katika shughuli nzima za kampeni.

Hapa kuna mgawanyiko mkubwa sana na ndipo hata usemi wa siasa ni mchezo mchafu unaanza kuota mizizi. Kuna wanasiasa ambao nguvu ya kifedha za kampeni hutokana na mifuko ya wananchi wenye moyo wa upendo na hamasa kushawishika wenyewe kushiriki kumchangia mgombea ambaye wanampenda aje kuwaongoza, jambo ambalo ni jema sana.

Wanasiasa kama hawa wakati mwingine huwa hawapendi kushiriki katika safu ya uongozi yaani kuwa viongozi lakini kipaji cha uongozi kinawafichua na kuwatambulisha kwenye jamii na wananchi kumshawishi ashiriki katika shughuli za siasa zitakazomuwezesha kuongoza.

Siasa za Marekani zinazoendelea hivi sasa kwa kampeni ndani na nje ya vyama tayari kuelekea ikulu ya nchi hiyo na kurithi kiti cha Raisi George W. Bush zinaweza kutufundisha mengi hasa katika shughuli ya namna ya kupata fedha kwa ajili ya kampeni, kwa uwepo wa asilimia kubwa ya uwazi juu ya vyanzo vya mapato na watu wanaochangia kwa wagombea.

Si Marekani tu, hata hapa nchini kwetu wapo wanasiasa ambao walichangiwa katika chaguzi tofauti tofauti hadi kuwa fikisha mahali walipo kwa kuhodhi madaraka na kuwatumikia wananchi hao.

Wapo vilevile wanasiasa ambao wameingia wakatumia fedha zao kama mtaji kuwekeza katika shughuli za siasa hasa kuendeshea shughuli za kampeni, hawa kuna mawili; mosi wanaweza kuwatumikia vyema wananchi lakini vilevile pili wanaweza wasiwatumikie vyema wananchi na kuwa makini katika kutafuta namna ya kurudisha fedha ambazo alitumia wakati wa kampeni.

Lakini kuna kundi la wanasiasa linalobebwa na baadhi ya matajiri, ambao wanawachangia kila shughuli na gharama za kipindi chote cha kampeni hadi kunyakuwa madaraka.

Kundi hili mara kwa mara linafanya hivi kupata kinga dhidi ya mali na hadhi yao katika jamii. Pia kuchochea hoja na kuweza kupenyeza hoja "ajenda" zao kwenye vyombo vya maamuzi kupitia wanasiasa hao.

Hapa ndipo tunaona baadhi ya wanasiasa kuwa mstari wa mbele kujenga hoja ambazo lazima upate wasi wasi kama ni kwa maslahi ya wananchi na taifa kwa ujumla ama kwa maslahi ya watu na kikundi kidogo.

Wapo wanasiasa matajiri wanaoingia katika siasa kulinda maslahi yao na pia kutafuta zaidi fursa za kibiashara. Hawa huwa wakijishughulisha sana mara kwa mara na shughuli za maslahi ya kibinafsi.

Makundi haya yote kushiriki katika siasa na kujinadi. Hapa wananchi kwa msimamo na ufahamu huweza kung'amua makundi haya na kujua nani hasa anawafaa baina ya kundi toka vyama tofauti vya kiasa linalowakabili hasa katika kipindi cha kampeni.

Kuna kipindi kulikuwa na ongezeko la wimbi la wasomi kukimbilia katika shughuli za siasa, hapa ikazua zogo na maswali mengi vichwani kwanini wasomi hawa waache maslahi yao na utume wao kukimbilia siasa kwani ualimu ni wito ati!

Kumbe kama wengi wanavyotazama kwa kizazi hiki kama siasa na hasa utawala ni mwanya wa kujinufaisha na kuneemeka na si utumishi kwa umma kama enzi zile za Nyerere. Enzi ambazo hakuna tofauti kati ya kiongozi na mwananchi wa kawaida katika suala la umilikaji mali.

Kwani tumesha shahudia viongozi wakiondoka madarakani wakiwa na mali za kawaida sana tofauti na kipindi hiki cha sasa ambacho wanasiasa waondokapo madarakani tayari kuna tofauti kubwa katika umilikaji mali kulinganisha na kipindi alikuwa anaingia.

Hii labda ni moja wapo ya madhara ambayo yanajitokeza sasa baada ya kulipa kisogo Azimio la Arusha na kulibeba Azimio la Zanzibar.

Kwani kwenye azimio la Arusha ambalo Mwl. Nyerere aliliasisi aliweza kuweka miiko na sheria ambazo zinawachunga viongozi katika utumishi wao kwa wananchi.

Kuna ugumu mkubwa sana ambao unawakabili hasa viongozi wa sasa kwani azimio la arusha ndilo lililoumba taswira halisi ya Tanzania bora yenye usawa na hasa siasa safi katika madaraka.

Kama tulivyosikia katika hotuba ya Raisi Mhe. Jakaya M. Kikwete uwepo wa fikra, hitaji la kuangalia upya kanuni na taratibu kwa viongozi hasa katika namna na mienendo ya utumishi kuangaliwa upya.

Hii inatokana na uchanganyaji wa shughuli kama siasa na biashara ambapo mhusika anapunguza ufanisi na hata uwepo wa usawa na haki hasa katika kugombea nafasi ya kuendesha biashara mahali fulani. Si tunakumbuka ya "mpanda farasi wawili………" ama ya "mshika mawili……..".

Ni mwanzo mzuri wa kung'amua hitaji la kanuni kama ambazo Mwl. Nyerere alishaziona na kuziweka katika azimio la arusha kwa kupitia maadili ya uongozi. Na alipooza zimepewa kisogo akaasa kwa maandishi yake mwenyewe katika kitabu cha "Uongozi wetu na hatma ya Tanzania".

Lakini kama usemi aliowahi kuusema Nabii Isaah bin Marium ama Yesu Kristo kwa wanafunzi wake "Roho iradhi ila Mwili udhaifu"![Mathayo 26:41]. Kuna uwezekano mkubwa wa uwepo wa uradhi katika roho ya baadhi ya viongozi kuenenda kufuatana na maadili ya uongozi tayari kuwatumikia wananchi lakini kunaweza kukakabiliwa na udhaifu wa mwili.

Udhaifu wa mwili kama hofu, mashaka, aibu kwa wanaokuzunguka kuweza kuikamilisha dhamira halisi ya kuleta mabadiliko ambayo yanahitajika kwa kuelekea kwenye Tanzania yenye maisha bora ambayo ni ahadi kwa watanzania.

Lazima maneno ya Dk. Stockman katika kitabu cha "An Enemy of the People" kilichoandikwa na Ibsen; "..the strongest man is the one who stand alone…"[mtu jasiri ni yule anayeweza kusimama pekee-tafsiri ikiwa ni yangu] yafikiwe na kutekelezwa ili kutenda na si kunena tu "Muungwana ni Vitendo na si maneno".

No comments: