"every generation must out of relative obscurity discover its mission and either fulfill it or betray it" ....Frantz Fanon
ADVERT
07 February, 2011
Katiba Moja, Nyumba Moja!
Kadiri kila kaya inavyojitahidi kuwa na kitabu kitakatifu kwa mujibu wa imani yao yaani aidha msahafu kwa waislamu ama biblia kwa wakristu, inafungua mlango wa kuwa na kitabu cha mamlaka ya kidunia. Katiba!
Kadiri kila wakati kaya ikiketi chini na kusoma kitabu kitakatifu kwa minajili ya kujiimarisha kiimani na kupanua maarifa ya “elimu ahera”. Ndivyo hivyo pia ilipaswa kaya zikae mara kwa mara na kusoma kitabu cha mamlaka ya kidunia. Katiba!
Licha ya uwepo wa maduka ya kitabu cha katiba, bado wananchi wachache wanamudu kuwa na nakala ya kitabu hicho muhimu kwa kuhakikisha haki na maslahi ya kila mmoja yanalindwa. Kuhakikisha maslahi ya nchi kwa ujumla yanasimamiwa.
Hata kwa shule za msingi na sekondari iwe za kata ama zisizo za kata bado sehemu kubwa kitabu cha katiba ni ndoto. Hata mmoja ya mfano hakuna!
Naye mwenyekiti wa kijiji ama mtendaji wa kijiji katiba kwake ndoto. Hata ofisi ya serikali za mitaa hakuna. Mwe!
Lakini maudhui ndani ya Katiba si kwa maslahi ya kila mwananchi? Maudhui yaliyomo si yanapaswa kuhubiriwa na kujadiliwa miongoni mwa kila raia? Ziwapi jitihada za kufikisha ujumbe uliomo ndani ya kitabu hicho cha kimamlaka?
Imeshapata kusemwa, haki haiombwi! Haki haipewi katika sahani kama pishi ya ubwabwa. Kila mwananchi, kila mwalimu, kila mtendaji wa serikali za mitaa ama kijiji anapaswa aweke juhudi ya dhati kuhakikisha anakuwa na nakala ya Katiba.
Kila shule ihakikishe inakuwa na nakala za kutosha za katiba. Kila mwanafunzi ahakikishe anapata wasaa wa kusoma aidha kwa mfumo wa makundi ama mmoja mmoja.
Kila kaya nchini ihakikishe ina nakala ya Katiba na iwe inatenga muda wa kusoma aidha kama kaya nzima ama kila mwanakaya kwa nafasi yake.
Kama vile tunavyojitahidi kujifunza masuala ya kiimani ndivyo hivyo pia tujitahidi kuwekeza katika kujifunza masuala ya kidunia hususan utendaji wa tawala, katiba na mantiki yake.
Kama tunavyopeana zawadi za vitabu ndivyo pia tuanze tamaduni ya kupeana zawadi ya kitabu cha “Katiba”. Tujitahidi pia hata kupeleka zawadi za Katiba kwa ndugu na marafiki zetu jijini na vijijini.
Baruapepe: michaeldalali@yahoo.com
© Michael Dalali, 2011
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment