By Michael Dalali
Uwakilishi ni moja ya msingi muhimu wa demokrasia. Demokrasia inasititiza katika watu kuwa nguzo kuu ya uendeshaji wa serikali na vyombo vyake kwa maslahi ya watu. Demokrasia ya uwakilishi (Indirect/Representative Democracy) inasisitiza zaidi uwakilishi wa makundi ndani ya jamii katika vyombo vya maamuzi na uendeshwaji wa serikali.
Katika kuelekea uchaguzi mkuu mwaka huu, tayari tumeanza kushuhudia makundi ndani ya jamii yakicharukia katika uwakilishi wao. Makundi kandamizwa yamekuwa yakijipanga dhidi ya makundi kandamiza. Wanasiasa wa makundi kandamiza wamekuwa wakitafuta mbinu za kuwashawishi wananchi wa makundi kandamizwa.
Tumeshasikia kauli kama; “serikali yangu itashirikisha vijana zaidi katika baraza la mawaziri”. Kauli ambazo zimeibua mjadala na kuhamasisha tafakari ya uwakilishi wa makundi katika vyombo vya maamuzi.
Licha ya ukubwa wa makundi mathalani ya wanawake na vijana kwa idadi, bado yamekuwa yakiwekwa chini ya ukandamizwaji kifikra na kimtazamo. Ndiyo tunasikia majina na kauli kama “makundi yaliyotengwa pembezoni” (marginalized groups), “vijana taifa la kesho” n.k
Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Vijana ya mwaka 2007,inatanabaisha kijana kama mtu mwenye miaka 15-35. Na kumaliza utata wa umri stahiki wa kundi hili.
Lakini makundi haya mathalani wanawake na vijana ndiyo msingi wa uzalishaji mali nchini na kwenye mataifa mengi duniani. Vijana wanahodhi asilimia 65 katika makundi ya uzalishaji mali. Lakini vijana ni chini ya asilimia 10 katika Bunge lenye wabunge 324. Wabunge wanawake wa kuchaguliwa wakiwa 22 tu.
Si katika uzalishaji mali tu, kundi la vijana na wanawake wanaidadi kubwa pia katika idadi ya watu nchini. Vijana kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2002, wanahodhi asilimia zaidi ya 35 katika idadi ya watu nchini. Je inatosha asilimia 35 kuwakilishwa kwa chini ya asilimia 10 katika vyombo vya maamuzi mathalani Bunge?
Ikumbukwe Katiba inatoa haki kila mwananchi kuchagua na kuchaguliwa kwa mujibu wa sheria. Kijana mwenye miaka 21 anaruhusa ya kisheria kugombea nafasi ya ubunge, udiwani.
Vijana ndiyo chachu na nguvu ya ushindi kwa wabunge wengi walio na wasio vijana. Lakini vijana bado hawajajiwakilisha wenyewe vya kutosha.
Wapo hata baadhi ya wabunge na viongozi wengine wa kisiasa ambao wanapenda kujibainisha kama ni vijana licha ya kuvuka ukomo wa umri wa ujana unaotambulika. Hii inadhihirisha tunu ya ujana katika kuchochea ustawi wa taifa.
Baadhi ya nchi wameweka mfumo wa kupata wawakilishi wa makundi katika jamii. Mathanali kundi la wanawake ambalo huwapata fursa ya kuwakilisha kupitia viti maalumu. Tanzania ipo katika mfumo huu. Lakini hatuna mfumo wa kuweka fursa ya uwakilishi kwa vijana. Ingawa nchi nyingine kama Uganda wanamfumo wa viti maalumu hadi kwa vijana. Vijana wanapata wawakilishi wa kundi la vijana ambao hupatikana kupitia baraza la Taifa la vijana lisilofungamana na itikadi za kivyama/kisiasa.
Tanzania bado haina baraza la Taifa la vijana wala mfumo rasmi wa viti maalumu kwa kundi la vijana. Baadhi ya vyama vya siasa vimejiwekea taratibu kupitia viti maalumu vya wanawake kupata wawakilishi kupitia vigezo vya makundi katika jamii mathalani uwakilishi toka asasi za kiraia, taasisi za elimu, walemavu, vijana n.k. Hapa ndipo wabunge kama Mhe.Lucy Mayenga na Hayati Mhe.Amina Chifupa wa CCM ama Mhe.Mhonga Said na Mhe.Halima Mdee wa CHADEMA walipata nafasi kuwa wakilisha vijana haswa vijana wanawake.
Bado vijana nchini hawajapewa fursa na msaada wa kutosha katika kugombea nafasi za uwakilishi katika vyombo vya maamuzi licha ya kuwa na uwezo. Vipo bado vikwazo vingi wanavyopata vijana kuelekea katika ushiriki wao kuwakilisha.
Uwezo, kipaji cha uongozi, ufahamu, fikra mbadala, misingi thabiti, maadili na uthubutu wa kijana wapaswa kuwa chachu na ngao katika kuvishinda vikwazo kama uzoefu wa kiutendaji, rasilimali fedha, kutokuwa na mke/mume wala watoto.
Ieleweke hatuhitaji tu kuongezeka idadi ya uwakilishi wa makundi ya wanawake na vijana katika vyombo vya maamuzi bali kupata wawakilishi bora na wanaofaa toka katika makundi haya.
Pia kuongeza idadi ya wawakilishi vijana katika vyombo vya maamuzi isiwe mbadala wa wawakilishi wachache makini wa makundi mengine kama wanaume waliopo. Bali iwe kuondoa katika jitihada za kupunguza uwakilishi hafifu wa wananchi. Kupunguza wawakilishi wengi ambao wapo kama hawapo hususan katika kuchangia ujenzi na ustawi wa Taifa.
Tukitathmini vijana wa miaka 21-30 wabunge wa kuchaguliwa katika bunge letu wapo idadi ndogo. Lakini tumeweza ona mchango mkubwa katika kipindi cha miaka ya 2005-2010 katika bunge namna ambavyo vijana wachache waliopo wa umri wa 21-30 walivyoleta tija katika uhai wa mijadala, maamuzi magumu, ujenzi na ustawi wa Taifa letu.
Hii inaleta faraja na kutoa mwanya wa ziada kwa wananchi kuwapa ridhaa vijana kuingia na kuongeza idadi ya uwakilishi katika vyombo vya maamuzi. Kuwapa fursa kutumia akili, nguvu na afya katika kujenga na kustawisha Taifa.
Vijana wanapaswa kutambua nguvu waliyonayo katika kufanikisha ushindi. Nguvu hizo za vijana zapaswa kuelekezwa pia kwa vijana wagombea makini, imara na wazalendo. Kusaidia kukuza ushiriki wa vijana katika vyombo vya maamuzi. Vijana waweze kuwakilisha ipasavyo na kutetea ajenda za vijana na za Taifa kwa ujumla.
Vijana ni sehemu kubwa na muhimu ya watanzania. Uwiano wa uwakilishi wa makundi katika jamii ni muhimu kuelekea ustawi na demokrasia hai.
Ewe kijana jitokeze ujiandikishe kwenye daftari la kudumu la kupiga kura. Tunza kadi yako ya kupigia kura. Jitokeze kugombea, shiriki, hamasisha, hamasika, piga kura na saidia vijana katika mchakato mzima kuelekea kukuza uwakilishi wa vijana katika ngazi zote za maamuzi kama ubunge na udiwani.
Wakati wa mabadiliko ni sasa, wahenga waliasa; “linalowezekana leo lisingoje kesho”.
Wasiliana: michaeldalali@yahoo.com +255 717 011 112
No comments:
Post a Comment