VIJANA WATANZANIA NA NADHARIA YA “NDIYO TUNAWEZA”!
Na Michael J. Dalali.
Moja ya nadharia ambapo wengine wanaweza ichukulia kama falsafa iliyoweza kuchukua umaarufu mkubwa na kuzaa matunda ni nadharia ya “Ndiyo Tunaweza” ama kama kwa lugha ya kimombo ya “Yes We Can” ambayo imeibuliwa na mwanasiasa mahiri na hatimaye Rais mteule wa nchi ya Marekani.
Nadharia hii inamchango mkubwa sana katika ujenzi wa taifa lolote na si Marekani tu ama si kwa ajili ya chama cha demokratiki pekee cha marekani.
Nchini Tanzania tumeweza kushughudia nadharia mbali mbali ambazo zimeweza kutekelezeka na kuwa na msisimko katika maisha yetu ya kila siku, mathalani falsafa za mwalimu Nyerere na nadharia zake kama “Ujamaa na Kujitegemea” ikiwa mchango wa mabadiliko kwa Taifa zima la Tanzania.
Nadharia ama falsafa nyingine huwa na kutumika kama misemo ingawa si lazima misemo hususan ya kusiasa ikawa na sifa za kuwa falsafa ama nadharia.
Vijana wa kitanzania wanamchango mkubwa sana wa kuishi nadharia ya “Ndiyo Tunaweza” katika kuchangia kuleta mabadiliko makubwa sana katika Nyanja mbali mbali ambayo hata kimazoea tunafikiri hayawezi kutokea.
Lakini tukumbuke mabadiliko mara nyingi huitaji watendaji wa kuyaleta, na mabadiliko kwa wakati mwingine hugharimu.Lakini mabadiliko yana uhumimu hasa katika kuelekea ustawi bora wa jamii hususan katika nchi yetu ya Tanzania.
Kwa makala hii itajikita katika muktadha wa mabadiliko ya kisiasa ambayo vijana wanaweza kuchochea katika kuyaleta na kuweza kufanya mabadiliko katika ustawi wa maisha si tu kwa vijana bali kwa Taifa zima kwa ujumla kwani hata Mwalimu alisha tuhusia kwamba maendeleo huja na kuchochea kwa uwepo wa “siasa safi”!
Kwa tathimini rahisi tunaweza kubaliana bado sana ushiriki na ushirikishwaji wa vijana hususan katika michakato ya kisiasa bado ipo finyu sana nchini Tanzania licha ya wao kuwa na asilimia kubwa sana ya asilimia 68 katika idadi ya watu nchini.
Tuchukulie umuhimu wa kujitolea kwa vijana katika mchakato mzima wa kisiasa mathalani katika kampeni na kuelekea uchaguzi. Kuna mwamko mdogo sana katika kushiriki kimadhubuti katika kampeni, uchaguzi na kusimamia zoezi zima la kiuchaguzi bila kujali itikadi ya chama!
Lakini ni katika kipindi hiki ndipo vijana wanaweza kupoteza maslahi yao kama wasipo kuwa makini kusimamia mchakato huu.
Mathalani tuchukue mfano; vijana tukimwona mgombea ambaye tunamwamini kwa uwezo wake na hoja anazotoa zikiwa na uhalisia na kuelekea kutatua changamoto kubwa sana zikabilizo Taifa twaweza kusimamia mchakato wa kuhakikisha usambaaji wa taarifa zake, kudhibiti uchafuzi wa siasa-propaganda, na hatimaye kushiriki katika kulinda kura zoezi ambalo linaweza hatimaye kumpata kiongozi safi na bora kwa ajili ya maendeleo toka ngazi ya vyama hadi taifa licha ya kujifunga kiitikadi wala chama.
Tumeweza ona na kusoma jinsi vijana wa marekani waliweza hata kuomba udhuru katika sehemu zao za kazi na kwenda kushiriki katika kulinda na kusimamia zoezi la upigaji na uhesabuji kura achilia mbali wachache ambao hata waliweza kuomba udhuru mapema na kushiriki katika kampeni.
Tunapaswa kujitoa katika kuyaelekea kuyapata mabadiliko ambayo tunayaamini hususan katika kufikia demokrasi ya kweli. Wakati ni sasa, na tushiriki ipasavyo katika kuyaleta maendeleo hususan katika Nyanja ya siasa, NDIYO TUNAWEZA!!
©Michael J. Dalali, 2008.
No comments:
Post a Comment