ADVERT

22 October, 2007

WASOMI NA MAONO YA TAIFA LETU

Taifa lolote hupokea maono mbali mbali kufuatana na matukio, kipindi juu ya hali halisi itakayo jiri ama inayoikabili.Watu wa ngazi mbali mbali hutoa maono hayo ingawa mara nyingi huwa wazee kwani wao huwa wanauzoefu na matukio mengi yaliyowahi kupata kutokea mahali pengi na hususan katika nchi yao hiyo.

Katika nyakati za sasa wasomi pia huwa na mchango mkubwa sana katika kutoa maono ya wapi hasa tunaelekea kufuatia uchunguzi, tafiti mbalimbali na upeo wao kutokana na kupevuka kielimu waliyoipata kwa muda mrefu na kujua mataifa mengine wamepitia njia zipi hata kuvuka baadhi ya changamoto zilizokuwa zinawakabili.

Magwiji ya uchumi huwa na msaada sana pale wanapodiriki kutoa ushauri na hata kukosoa na ikibidi kukemea kama wakiona hali ya uchumi inachezewa na kupelekwa “kishengere nyuma” kwani wanautaalamu na upeo mkubwa katika nyanja hiyo.

Vilevile kwa wataalamu wa mambo ya sheria wanaweza kuona wazi hali ya uchezewaji wa kisheria na ufinywaji wa demokrasia hivyo kuwa na nguvu ya kiutaalamu kukosoa na kukemea huku wakisaidia kwa kutoa njia mdabala hasa nini kifanyike kuokoa jahazi na kuhakiki ugawaji wa haki katika jamii na heshima ya katiba na sheria mbalimbali.

Wataalamu wa siasa na mambo ya utawala na uundwaji wa sera wanamchango mkubwa sana pale taaluma yao inapotumiwa pasi kuegemea vionjo vyao vya mioyoni kwa mapenzi ya itikadi ya chama fulani hivyo kusaidia kuboresha ustawi wa siasa na utawala bora ambavyo ni misingi mikubwa sana katika kuleta uimara wa demokrasia na maendeleo ya Taifa.

Kuna kipindi ambacho kuligubikwa na wimbi la matumizi mabaya ya nguvu hii ya kitaaluma [ingawa inawezekana baadhi wanaendelea] na kuchochea matakwa binafsi ili wahusika waweze kujijenga vyema hasa katika maisha bora binafsi kwa kukiuka maadili na kusaliti tumaini la wananchi kwa kundi hili la wataalamu kuwa ni watu wa kuaminiwa kwa kile watakachokisema na kushauri.

Kusaka huku kwa maisha ubora wa maisha binafsi zaidi n a kukosa moyo wa kuridhika kulifanya uwepo wa wimbi kubwa la wanataaluma hawa “wasomi’ kuikimbilia medani ya siasa na kusaka madaraka huko na kukubali hata kufanya mambo tofauti nay ale waliyofundwa alimradi wanalinda itikadi walizozikimbilia kujineemesha.

Hapa ieleweke kuwa “nongwa” inakuja pale msomi anapohusika katika kuwaaminisha wananchi wanaoheshimu fikra za kisomi baada ya kuona majina kama “profesa” ama “daktari” kuwa ‘Nyeusi” ni “kijani”! wakati uhalisia nyeusi ni nyeusi na kijani ni kijani ama umaskini si umaskini bali ni maisha bora.

Na hapa wanakuwa wamechangia kwa kiasi kikubwa kuwakwaza wananchi amabo ni kama wadogo mbele yao.Ikumbukwe vitabu vitakatifu vimeandika adhabu ya watu kama hawa ni kufungiwa jiwe la kusagia shingoni na kutoswa katika kilindi cha bahari [Mt 18:06 au LK 17:1-2]

Wasomi wanaupana wa kutumia vyema vyombo vya upashanaji habari kama radio, televisheni, magazeti, mitandao kuelezea fikra zao, taaluma inavyosema juu ya mambo mbali mbali na hata kutuhabarisha ukweli na undani wa maono kutokana na tafiti mbalimbali ambazo huziendesha mara kwa mara ili kuwahabarisha na kuwaelimisha wananchi ambao wanakiu ya ufahamu.

Mihadhara ya wazi na midahalo pia ni namna ambayo wasomi wanaweza kuitumia vyema sana kwa manufaa ya kuelimisha umma nini hasa kinaendelea na njia gani tuifutae kuelekea kwenye uwokovu wa kimaendeleo nchini.

Msomi anayethubutu kusimamia maadili na taratibu za kisomi za kuelimisha yeyote mhitaji elimu sahihi naamini anatimiza wajibu wake vyema na hata kama kupata dhawabu kwa Mungu kutokana na kutimiza vyema utume basi atakuwa miongoni mwa wabarikiwa na wanaochangia maendeleo bora ya kupambana na hali ngumu inayolikabili taifa hili.

Nilibahatika kuhudhuria kumbukizi ya Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius K. Nyerere iliyofanyikia Chuo Kikuu Cha Dar-Es-Salaam eneo la Mlimani siku ya kitaifa ya kumkumbuka Mwalimu tarehe 14 mwezi huu wa Oktoba.

Kumbukizi hiyo iliyounganisha na kuwakutanisha wanafunzi, walimu [huwa wanafurahi sana wakiitwa “wahadhiri”], wanaharakati, wanasiasa, wanahabari, wanadiplomasia na watu wengine wengi mashuhuri pasi kuwasahau wananchi wa kawaida akina siye.

Hapa niliweza kuibua mambo mengi sana yanayoendelea katika Taifa letu hususan vyuo vyetu hapa nchini.

Niliweza kuona muongozaji akihusika kwa kiasi kikubwa kuminya baadhi ya washiriki kutoa maoni yao na duku duku yaliyopo moyoni adharani huku waratibu wakuu wakiendelea kuangalia tu bila kukemea tabia ile.

Waliokuwa waathirika zaidi ya tabia hii mbaya walikuwa wanafunzi ambao kila wakitaka kuongea na kugusia mambo ya msingi ya ukweli yaliyotokea wakiyahusianisha na Mwalimu Nyerere mratibu aliingilia kati na kutisha hivyo hata kupoteza mtiririko wa waongeaji hawa waliokuwa na hoja mbali mbali.

Nikaanza kujiuliza hivi hapa nani hasa analindwa? Nani hasa anafichwa asipate ukweli huu ama maoni haya? Na ni kwanini basi wameandaa na kuweka muda wa uchangiaji wa mada ama maoni?

“Bora wange andaa DUPSA bwana hawa jamaa makada kweli” ni moja ya kauli niliyoisikia toka kwa mwanafunzi aliyekuwa karibu nami.Bila shaka wanafunzi walisha anza kuona wanaonewa hadharani wa waandaaji wa tukio lile kwa kuwanyima uhuru wa kuongea na kuikumbuka taasisi yao ya wanafunzi wasomao sayansi ya siasa na utawala [DUPSA] inayowapa fursa kujadili mambo kinaga ubaga.

Hapa nikakumbika namna ambavyo asasi mbali mbali nchini makini zinazotimiza wajibu kama asasi zisizo za kiserikali zinavyochukiwa na serikali kutokana na kuwa wazi na kusema ukweli yaani kudiriki kusema mfano tupo katika lindi la umaskini uliokithiri na si maisha bora.

Hapa wakaingia wasomi na watu mashuhuri nchini ambao wao waliongea waziwazi bila kuogopa wala kukatishwa na muongozaji.Hii ikazidi kuibua maswali mengi kichani.Kama hapa adharani peupe pee wasomi hawa wachanga wanakatishwa na kuzibwa midomo iweje pale wawapo katika vyumba vya mihadhara “madarasani” na semina? Kweli hali ni shwari? Utoaji wa elimu yetu ni huru kweli ama inaficha na kulinda mawazo fulani yasitapakae kwa wadhibiti makada wenye kinga ya uhadhiri?

Moja ya wahadhiri wa siku nyingi na gwiji la sheria alikuwa wazi kutoa duku duku lake na hofu hasa wapi taifa linaelekea, hofu ambayo hata baadhi ya wadau nchini walishaiweka wazi lakini imekuwa ikipokelewa na majibu ya ajabu ajabu yasiyotosheleza uzito wa swali na mara nyingine lawama kutupiwa wapinzani kuwa ndiyo wanao makinisha wananchi kuuliza maswali mazito kama hayo ya dira ya taifa ni ipi hasa.

“Nini chanzo zha haya mabadiliko toka ujamaa na sijui kwenda wapi?...ubepari si ubepari na kama ni ubepari wa kitapeli….kutoka haki ya Mungu kwenda haki ya mtu” msomi huyo akadokeza kuwa yupo katika hatua za mwisho wa tafiti yake, nina hamu maono ya utafiti huo yakianikwa kwa wananchi nao wamakinike.

“Kuelewa vyema migongano ya maslahi ya kimatabaka utasaidia kuelewa vyema hali ya hivi sasa.Je msukumo huo ndiyo umechangia katika mabadiliko toka haki ya Mungu hadi haki ya mtu?

Aliendelea kutoa hoja kwa kuhoji na kuleta msisimko wa ajabu ubongoni na mshtuko moyoni mwa vijana chipukizi wasomi.

“Tunasema hatuna dira, MKUKUTA siyo dira? Visheni 2015 siyo dira? Maisha bora kwa kila Mtanzania siyo dira? Yote haya siyo dira!! Maisha Bora kwa kila mtanzania inaweza kuwa mradi wa mtu ama kikundi Fulani.Unaweza kuona kabisa nani atafanikiwa katika mradi huo.Taifa zima haliwezi kuwa omba omba hiyo siyo dira. Kuna tofauti kubwa sana kati ya mradi “project” na dira “vision” kwa manufaa ya watu na si mtu mmoja mmoja ama kikundi fulani”.

Msomi huyo akahitimisha kwa swali ambalo linahitaji mjadala mpana sana kuwa tunaweza kuwa na dira ya kitaifa yenye kusimamia na kutoa maslahi kwa matabaka yote katika jamii?
Alikuwapo pia mwanahabari wa siku nyingi na mtu asiye thubutu kuanika hadharani fikra zake hata kama zinahatarisha maslahi ya kundi fulani ambaye aliweza kumakinisha vijana wasomi na fikra yakinifu.

Naye aliweza kudokeza swala la sera kwa kukemea wale ambao wanadhani amani ni sera wakati uhalisia ni matunda ya utekelezwaji wa sera bora.Hivyo pasipo kuwa na sera bora yenye kutekelezwa kuna hati hati ya kuendelea kuwepo kwa amani inayopigiwa debe kama sera!

Hapa tunaweza kuona mantiki yake endapo huduma muhima za kijamii kama afya, elimu bora, maji safi, miundo mbinu vyote vinakuwa duni ndani ya Taifa lenye rasilimali za kutosha zaidi hata ya baadhi ya mataifa tajiri duniani.Lakini cha zaidi wakati wengine wakitaabika lipo kundi la watu wachache linaloneemeka kwa rasilimali na ulinzi mkubwa wa nyadhifa mbali mbali wanazohodhi.

“Tunaona watawala wanaozani mabavu ndiyo njia pekee, sehemu nyingine inapaswa watumie japo busara kidogo na kuruhusu nafsi kusikiliza mawazo tofauti na yake.”

Viongozi kama hawa ni waoga na wakandamizaji.Mwoga anaona wakipata uhuru wa kuzungumza hana ujasiri wa kupinga kwani hana hoja.

Hapa tunaweza kuona baadhi ya wanachama wanavyohangaika kuzunguka mikoani nao ati kujibu mapigo ya wapinzani ambao walikuwa watimiza wajibu wao wa kuwaelimisha wananchi juu ya hali halisi ya ufinyu wa haki katika ugawaji wa mapato ya rasilimali za Taifa letu hili na namna ambavyo ufisadi unavyolipeleke shimoni.

Kwa utendaji bora kufuatana na taratibu za utumishi wa umma ungeweza kuepusha mambo yote haya na kuingia kwa gharama zisizo za msingi na purukushani za hapa na pale.

Kwa ujasiri wa kutopiga kura kisa unatetea chama pasi uhalisia wa hitaji katika kutetea kutokana na ufinyu wa hoja katika jambo lenyewe, ukosefu wa ujasiri pia kwa kiranja mkuu wa mijadala katika jumba tukufu linalikutanisha watu wa itikadi na falsafa za vyama tofauti vyote vinachangia “magoli” haya kuwa mengi zaidi ya yalivyotarajiwa.Hapa hakuna cha kupoteza fedha kwenda bagamoyo walozi wamejaa ndani ya nyumba na kizuri wanajulikana ila wanaonewa soni tu!Yaani hata maswahiba wenzao walivyo wasaidia kuwataja [list of shame] bado wanajifanya kubisha astahk-filulah!Kweli sikio la kufa halisikii dawa.

Vituko zaidi tunaona hata katika baadhi ya sehemu kama vyuoni na mahala pengine ambapo tulitegemea uhuru wa kupata taarifa na kuwa na fursa ya kujadiliana katika hoja kumepenyezwa makada wenye kulinda uhuru huu kwa nguvu, kwa kutumia vyombo vya dola kama FFU kuzuia watu kutoa mawazo.

Mwalimu Nyerere alikuwa na ujasiri wakufikiria na kuona kule ambako wengine hawataki kuona ama kufikiri.Hawa ndiyo aina ya viongozi tunaowakosa hivi sana,wanaozani kuwatoa watu makini katika jengo la kutungia sheria na kuwaziba midomo katika maeneo yaliyojaa makada wao ndiyo wanawaziba wananchi kupata maumivu ya hali ngumu ya maisha inayoletwa na kukithiri kwa ufisadi na utawala mbovu.

Wananchi wanamaswali mengi sana ambayo yanahitaji majibu tena haraka sana!hawana haja tena na sifa za kujipa wenyewe ndiyo matokeo yake viongozi tena wa juu wanaambulia kuzomewa na hata kuvurumushiwa mawe!

Watanzania siyo wajinga kabisa wala si kwamba hawaelewi mambo yanayoendelea na namna ambavyo wanafanyiwa sivyo ndivyo ila ni waelewa na watu ambao wanakubali kueleweshwa.Tusiendelee kuwanyanyasa kisa eti ni watulivu.Siku wakiamua na kuamka watakumbushia machungu yote ya nyuma na hapo ndipo tutaelewa nini umuhimu wa utawala bora na utekelezwaji wa sera nzuri kwa vitendo.

Ni heri kuuwahi udongo ungali mbichi na kutilia umakini maneno ya Raisi wa Nigeria Musa Yar’ Adua “Serikali ni lazima ijipatie sifa yake, heshima yake na madaraka yake kwa tabia yake na ile ya viongozi wake.Na tabia hiyo ni uaminifu, uadilifu, ukweli, uwazi, uwajibikaji na uwezo wa kutimiza ahadi ambazo zinatolewa kwa wananchi.Bila hayo hakuna serikali inayoweza kuheshimiwa na wananchi”.

Mwandishi wa makala hii ni mwanaharakati na Katibu Mkuu wa asasi ya dira ya vijana TYVA.Anapatikana kwa namba: 0755-459783 na barua pepe: michaeldalali@yahoo.com.

No comments: